Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi (NEC), inatarajia kukutana Desemba 13, mwaka huu jijini Dar es
Salaam, imefahamika.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam
jana na Kaimu Msemaji wa chama hicho, Seleman Mwenda, ilisema mkutano huo
utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), kitakachofanyika Desemba 11 hadi 12,
jijini Dar es Salaam.
Ingawa hadi sasa ajenda za vikao
hivyo hazijajulikana, lakini wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema,
kufanyika kwa vikao hivyo kunatajwa kuwa ni mkakati wa Mwenyekiti wa chama
hicho, Rais Dk. John Magufuli kutaka kuisuka upya CCM.
Baadhi ya wachambuzi hao wanasema
uteuzi wa wajumbe watatu wa sekretarieti ya chama hicho kuwa mabalozi ni
mwendelezo wa mkakati huo kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho
mwakani.
Mbali na hao mjumbe mwingine wa
sekretarieti, Dk Asha -Rose Migiro aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini
Uingereza na nafasi yake ndani ya chama kuchukuliwa na Pindi Chana ambaye naye
ameteuliwa kuwa balozi.
Katika Serikali ya awamu ya nne,
Pindi Chana alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na
baadae mwaka huu aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na
Uhusiano wa Kimataifa.
Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Dk.
Emmanuel Nchimbi, kuteuliwa kuwa balozi kunathibitisha kuhusu uwapo wa mkakati
wa Rais Magufuli kusuka upya chama hicho kwa kuweka sura mpya.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Nape Nnauye ambaye pia ni Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama
hatarajiwi kuwapo katika safu hiyo mpya, kwani tayari yupo serikalini.
Mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho (Bara), Rajabu Luhwavi ambaye ameteuliwa kuwa balozi anazidi kutoa
taswira kuhusu mkakati wa Rais Magufuli kusuka upya chama hicho.
Katika hotuba ya Rais Dk. Magufuli
baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho alisema miongoni mwa mambo
atakayoyatekeleza ni kuimarisha utendaji kazi wa chama, huku akimnukuu hayati
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kusema kuwa chama legelege huzaa
serikali legelege.
“Nitashirikiana nanyi kujenga chama
madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo
majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya katiba na kanuni zetu ili kukidhi
mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo.
“Tutahakikisha pia tunakuwa na safu
bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia shina hadi taifa. Tutaangalia muundo
(structure) wa chama chetu katika ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa
na tija katika chama na hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi” alisema Dk.
Magufuli.
Dk. Magufuli alihoji kuhusu uhalali
wa kuendelea kuwapo vijana wa chipukizi ndani ya chama hicho pamoja na baadhi
ya safu za uongozi ndani ya chama hicho.
“WanaCCM ni lazima tujiulize je ni
kweli katika zama hizi bado tunahitaji mtoto wa miaka 8 hadi 15 kuwa chipukizi
kwa ajili ya kumtumia kwenye siasa badala ya kumwacha asome? Kama akiwepo
chipukizi wa CCM, chipukizi wa NCCR au Chadema ama TLP tutakuwa tunajenga nchi
ya namna gani?
“Je bado kuna umuhimu wa kuwa na
makamanda wa vijana ambao mara nyingi wenye kupewa vyeo hivyo ni wale wenye
uwezo wa kifedha pekee? Je walezi kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) bado
wanahitajika? Je washauri ndani ya Jumuiya ya Wazazi wanahitajika?"
No comments:
Post a Comment