Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema
anamshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuruhusu vikao vya ndani.
Amesema vikao hivo, “ni
vitamu zaidi kuliko vile ya nje.”
Hayo aliyasema Dar es
Salaam alipofungua mafunzo ya siku mbili kwa madiwani, wabunge na viongozi wa
Chadema Mkoa wa Dar es Salaam yanayoendelea kutolewa na Shirika la Konrad
Adenauer Stiftung (KAS) la Ujerumani.
Akizungumzia ziara za
kanda zilizofanywa na viongozi wa chama hicho hivi karibuni, Lowassa
alisema vikao vya ndani vimewapa nafasi na muda mwingi wa kuzungumza na
wanachama kwa karibu zaidi.
“Tumefanya ziara, tumeona hali ya
barabara ni nzuri lakini hali ni nzuri zaidi tulivyozungumza na wanachama wetu
na tunamshukuru Rais.
“Aliona hakuna haja ya mikutano ya
nje akatupatia vikao vya ndani, Loh! Ni vizuri, ni vitamu zaidi kuliko vile vya
nje.
“Tunapata nafasi nzuri ya
kuzungumza na wanachama ana kwa ana, kwa muda mrefu kwa mapenzi na mahaba.
“Nataka niwaambie Chadema ipo imara
sana. Watu walidhani wamekata tamaa lakini wapo imara katika kuhakikisha chama
kinapata ushindi mwaka 2020,”alisema Lowassa.
Alisema yapo malalamiko madogo
madogo likiwamo watu wengi kutaka uongozi wa chama.
Alipendekeza yawepo mabadiliko
katika katiba ya nchi kuongeza nafasi za uongozi.
“Wana malalamiko madogo madogo
lakini mengi ni ya uongozi, kila mtu anataka kuwa kiongozi hadi nikakumbuka
kule Kenya walipobadilisha Katiba wakaongeza nafasi za uongozi, magavana,
mameya na nyingine ili zipatikane nafasi za siasa za kuongoza na mimi
nadhani tungepata muda tufafanue katiba ili ziongezwe nafasi za uteuzi.
“Au mnaonaje?” Lowassa
aliwauliza wajumbe ambao kwa pamoja waliitikia: “Ndiyoo”
Alisema kuna kila dalili ya Chadema
kushinda uchaguzi wa 2020.
Aliwataka viongozi wa chama
hicho kushikamana na kuepuka maneno ya kuwagawa akisisitiza kuwa bila
mshikamano hawataweza kushinda uchaguzi ujao.
“Dalili zote zinaonyesha tutashinda
lakini kama tutakuwa wamoja.
“Bila umoja hatuwezi kushinda na
CCM wanajua maana ya umoja ndiyo maana wanasema umoja ni ushindi, hivyo maneno
ya kutugawa tusiyakubali, viongozi tushikamane,” alisema
Lowassa.
Alitaja mbinu nyingine ya ushindi
kuwa ni kwenda vijijini kutoa elimu kwa sababu utafiti unaonyesha kuwa CCM
imekuwa ikishinda maeneo yaliyo nyuma katika elimu.
“Wakati tukiwa Dodoma kwenye ziara
kuna vijiji mtu anakuambia mimi nampigia kura Nyerere (Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere), na akiona polisi anakimbia.
“Sasa kama mtu anakimbia akimwona
polisi anawezaje kulinda kura? Hivyo bila kwenda kutoa elimu vijijini
hatuwezi kushinda,” alisisitiza Lowassa na kuongeza:
“ ‘There is no time left’ (Hatuna
muda wa kupoteza), muda uliobaki ni mdogo sana hatuna budi kuutumia
vizuri kwa kuangalia wapi tulikosea na turekebishe vipi na tuongee kutoka
moyoni tusiogopane.
“Tukosoane bila kusingiziana na
tuone muda uliobaki tunafanya nini ili tushinde,” alisema
Lowassa.
No comments:
Post a Comment