Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amemuagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kuwasimamisha kazi
maofisa waandamizi watano wa mfuko.
Maofisa hao ni wanaosimamia mpango
huo pamoja na Meneja wa Uratibu na Mkurugenzi wa Uratibu kutokana na kushindwa
kusimamia mpango wa kunusuru kaya masikini.
Kairuki alisema maofisa hao ndio
viongozi wasimamizi wakuu wa mpango huo katika Awamu ya Tatu ya Tasaf na
wamesimamishwa kupisha uchunguzi wa jinsi walivyohusika kuvuruga utekelezaji wa
mpango huo hadi kufikia kuandikisha kaya zisizo na sifa ufanyike.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Dar es Salaam, Kairuki alisema ameshauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na tayari ameshaelekeza
waratibu wa Tasaf wa wilaya pia wasimamishwe kazi.
“Nimemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji
wa Tasaf awasimamishe kazi mara moja na kuendelea na hatua nyingine za kinidhamu
dhidi ya maofisa washauri 106 walioko kwenye halmashauri walioshindwa
kufuatilia na kusimamia mpango huu mpaka kusababisha kaya zisizostahili
kuingizwa kwenye mpango na kuendelea kulipwa isivyostahili,” alisema Kairuki.
Aidha alisema ameagiza ufanyike
uchunguzi wa kina kubaini ushiriki wa maofisa hao na kuchukua hatua stahiki kwa
wale watakaothibitika kuhusika.
Aidha ametaka uchunguzi huo
ukamilike ndani ya mwezi. Karuki alisema baada ya uhakiki kufanyika kaya 55,692
zimeondolewa kwenye mpango kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kaya
kuhama kijiji, kutojitokeza mara tatu mfululizo kupokea ruzuku, kuwa wajumbe wa
kamati mbalimbali, wastaafu, viongozi na watumishi wa umma.
Alisema kuanzia Januari 2014 hadi
Septemba 2016, Sh 6,427,110,309 zimeokolewa kwa kaya 42,035 zilizoondolewa kwa
kipindi hicho na kwa kuwa kazi hiyo ni endelevu kuanzia Oktoba 2016
wakikamilisha kuziondoa kaya zisizostahili kiasi hicho cha fedha kinaweza
kubadilika.
Hata hivyo amewaagiza Tasaf
kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na halmashauri kuongeza udhibiti wa fedha
wakati wa malipo na kuhakikisha fedha zinalipwa kwa kaya zenye sifa peke yake.
Aidha, amewaagiza Tasaf kuendelea
kushirikiana na halmashauri zote kukamilisha kazi ya uhakiki wa nyumba kwa
nyumba katika halmashauri zote nchini kabla ya malipo yanayofuata ya Januari/
Februari 2017 kufanyika.
No comments:
Post a Comment