Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imesema
itazifutia usajili shule zote binafsi, ambazo zitabainika kukiuka agizo la
serikali la kuzitaka shule zote nchini kuwa na mihula miwili ya masomo badala
ya mitatu, ambayo imekuwa inafuatwa na shule zisizo za serikali.
Kaimu
Kamishna wa Elimu, Venance Manori alisema wizara yake ilitoa waraka huo ikiwa
ni njia ya kukazia Waraka wa Serikali Namba 5 wa Mwaka 2012 ambao ulikuwa
unaelekeza mihula ya masomo kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu, ifanane
ili kuepusha usumbufu kwa walimu na kwa wanafunzi.
Waraka huo ulifafanua kuwa kila
muhula utakuwa na likizo fupi na likizo ya mwisho wa muhula na siku za masomo
kwa mwaka zitakuwa ni 194. Pia waraka huo unataka siku za michezo ya
Umitashunta na Umiseta kwa shule za msingi na sekondari, zifanane kwa shule
zote. Lakini pamoja na kuwepo waraka huo, baadhi ya shule zisizo za serikali
zimeendelea kufuata mihula mitatu.
Baadhi ya shule katika ripoti za
wanafunzi za mwezi Disemba kwenda kwa wazazi, wameonesha kuwa mwaka ujao wa
masomo utakuwa wa mihula mitatu na nyingine minne.
“Wizara ilifanya utafiti na
kujiridhisha kuwa haiwezekani shule zinazotoa elimu msingi kuwa na mihula
mitatu, ndio maana tukataka nchi nzima tuwe na mfumo ambao unafanana ili
kuepusha usumbufu kwa walimu na wanafunzi,” alisema Manori.
Alisema kwanza haamini kama kuna
shule ambazo sio za serikali ambazo bado zinafuata mihula mitatu, na akaongeza
kuwa kama zipo na wizara hiyo ikapata uthibitisho, lazima hatua za sheria
zichukuliwe na hatua mojawapo ni kuzifuatia sheria.
“Ule waraka ulisambazwa kwa mamlaka
zote za utekelezaji ukiwemo umoja wa shule binafsi na taasisi inayosimamia
shule za dini ya Kikristo na shule za Baraza la Kiislamu, hivyo hakuna
kisingizio cha mtu kutopata huo waraka, hivyo lazima wautekeleze,” alieleza Manori.
Hata hivyo, pamoja na waraka huo
baadhi ya shule binafsi, zimekaidi agizo hilo na zimeendelea kufuata mihula
mitatu, jambo ambalo ni kwenda kinyume cha maagizo hayo ya serikali. Kutokana
na ukaidi huo, Manori alisema kuanzia mwakani, shule ambazo zitabaini kukaidi
agizo hilo zitafutiliwa usajili.
Manori alisema wakaguzi wa elimu
hiyo ndio kazi yao kuhakikisha kwamba maagizo yote ya serikali yanafuatwa. Pia
alitoa mwito kwa wazazi ambao wanapata maelekezo ya mihula ya shule inayoenda
kinyume cha maagizo ya serikali, waripoti suala hilo kwa malofisa elimu wilaya
na wakaguzi wa shule.
“Sio kwamba wazazi wote waje hapa
wizarani kulalamika, wale wanaoweza walete malalamiko hayo na walioko mikoani
waende kwa maofisa elimu wa mikoa, wilaya na wakaguzi wa shule ili hatua
stahiki ziweze kuchukuliwa,” alifafanua Kamishna huyo.
Alisema hivi karibuni wizara yake
itatoa kalenda ya masomo na mihula, itakayofuatwa na shule zote zinazotoa elimu
msingi, kama walivyotoa kalenda ya masomo katika mwaka huu.
Pia alikiagiza Chama cha Wamiliki
wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Baraza la Waislamu Tanzania
(Bakwata), Tume ya Huduma za Kijamii ya Kikristo ambao ndio wanasimamia shule
ambazo sio za serikali nchini, kuhakikisha wanachama wao wanatekeleza waraka
huo wa serikali.
Msimamo wa Tamongsco Katibu Mkuu wa
Tamongsco, Benjamin Nkonya alipoulizwa kutoa maoni yake alisema, “Niko kwenye
mkutano, lakini sisi bado hatukubaliani na waraka huo wa serikali, nitumie
e-mail yako nitakuandikia sababu za kupinga waraka huo.”
Hata hivyo, Nkonya baadaye alituma
nakala ya barua iliyoandikwa na yeye kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kumwomba shule binafsi ziendelee
kutumia mihula mitatu kwa sababu inarahisisha ukusanyaji wa ada kutoka kwa
wazazi na walezi.
BY: EMMY MWAIPOPO
CHANZO: HABARILEO
No comments:
Post a Comment