Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Utafiti wa Viashiria vya Virusi vya
UKIMWI (VVU) na Maralia (THMIS) wa mwaka 2011/2012 kwa upande wa Tanzania Bara
vinaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanawake wameambukizwa ugonjwa huo kuliko
wanaume.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista
Mhagama alisema takwimu zilizopo sasa zinaonyesha kuwa asilimia 6.2 ya wanawake
wameambukizwa ugonjwa wa ukimwi ikilinganisha na asilimia 3.8 ya wanaume.
Waziri Mhagama alisema kuwa
kutokana na utafiti huo, maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa upande wa Tanzania
Bara ni asilimia 5.3 na inakadiriwa kuwa jumla ya watanzania
1,538,382 wanaishi na VVU ambapo vijana wenye umri kati ya 15-24 ni asilimia
10.6 na watoto walio chini ya miaka 15 ni 11.8.
“UKIMWI bado ni janga kubwa nchini
Tanzania kwani takwimu zinaonyesha kuwa maambukizo mapya yanakadiriwa
kufikia watu 48,000 kwa mwaka hali ambayo inaashiria kupoteza nguvu
kazi kubwa katika nchi yetu”
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama
alisema Tanzania itendelea kushirikiana na nchi nyingine Duniani kuhakikisha
wanatokomeza janga la ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea
kuwahamisha wananchi waendelee kujitokeza kupima afya zao ili wajitambue na
kujua namna ya kujilinda kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza nchi
wanachama kuwaanzishia dawa mara moja watu wote watakaopima na kugundulika kuwa
na VVU.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dr. Leonard Maboko alisema kuwa kwa mwaka
2015 walioambukizwa VVU walikuwa Watanzania 2,100,000 ambayo ni idadi kubwa
ukilinganisha na idadi ya sasa lakini pamoja na kushuka kwa idadi hiyo
wananchi wanatakiwa kuendelea kujilinda mara dufu.
”Ingawa maambukizi ya VVU yameshuka
kutoka Watanzania 2,100,000 hadi 1,538,382, Watanzania hatutakiwi kubweteka
bali tunatakiwa tufanye jitihada za pamoja kuhakikisha janga hili linafikia
mwisho,”alisema Dr. Maboko.
No comments:
Post a Comment