Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) anatarajiwa
kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Afrika na Korea
unaotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba, 2016 mjini
Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano huu ambao umeandaliwa na
Serikali ya Korea kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika una lenga kukuza
ushirikiano pamoja na kuandaa maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Korea na
mataifa ya Afrika katika miaka mitatu ijayo.
Tanzania ni moja ya nchi nne (4) za
Afrika ambazo Korea imezichagua kuanzisha mahusiano ya kimkakati “strategic
partnership” yatakayozifanya nchi hizo kupewa kipaumbele katika kupokea misaada
na mikopo nafuu kutoka Korea katika kipindi cha miaka mitano ijayo kati ya 2016
hadi 2020.
Katika kipindi hicho Tanzania
itapokea kiasi cha dola za Kimarekani milioni 300 ikiwa ni asilimia 17.1 ya
msaada utakaotolewa Barani Afrika, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi
inayoongoza Barani humo kupata msaada wa Jamhuri ya Korea.
Pamoja na ushiriki kwenye Mkutano
huo, imependekezwa ufanyike mkutano baina ya Tanzania na Serikali ya Korea
kuzungumzia masuala ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.
Aidha, ushiriki wa Tanzania kwenye
mkutano wa Afrika na Korea ni fursa muhimu ya kukuza mahusiano baina ya nchi
zetu mbili hususan katika Nyanja ya uchumi. Serikali ya Korea ilitoa ahadi ya
kuongeza uwekezaji Barani Afrika hususan katikasekta za nishati, miundombinu na
viwanda.
Itakumbukwa kuwa, tayari Jamhuri ya
Korea inashirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo
Mradi wa kuendeleza kilimo cha Mwani Zanzibar wenye thamani ya Dola za
Kimarekani milioni 3.6 na Awamu ya Pili ya Mradi wa kuboresha Uchunguzi wa Afya
ya Uzazi Jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni nne
(4).
Miradi mingine ambayo Jamhuri ya
Korea inashirikiana na Tanzania ni ujenzi wa Daraja la Selander Jijini Dar es
Salaam, Mradi wa Daraja la Kikwete kwenye Mto Malagarasi Mkoani Kigoma na
Ujenzi wa Hospitali ya Kimataifa iliyopo eneo la Mloganzila Jijini Dar es
Salaam.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 01Desemba, 2016.
No comments:
Post a Comment