Mkazi wa kijiji cha Chapakazi, Mbalizi mkoani Mbeya, Jonas John (28)
anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapo, baada ya kukamatwa akifukua kaburi
la mtu mwenye ualbino, aliyefariki a kuzikwa kijijini Mumba mwaka 2010.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari, alisema John alikamatwa katika
kijiji Mumba kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati Wilaya ya Kipolisi Mbalizi,
mkoani humo saa 7 usiku jana.
Kijana huyo alikamatwa na askari
akiwa na wenzake wawili, wakifukua kaburi la mtu aliyefahamika kwa jina la
Sister Osisara, aliyekuwa mlemavu wa ngozi (albino) kwa lengo la kuchukua
viungo vyake.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikutwa
na majembe na koleo, ambayo walikuwa wakiyatumia kufukulia kaburi hilo usiku
huo, kabla ya wakazi wa maeneo ya jirani na makaburi hayo kubaini kilichokuwa
kikiendelea na kutoa taarifa.
Alisema baada ya mtuhumiwa
kukamatwa na kuhojiwa na polisi, aliwataja washirika wenzake wawili, ambao
walikimbia baada ya kuwaona askari. Kamanda Kidavashari alisema msako
unaendelea, kuwatafuta watuhumiwa wawili waliokimbia.
“Wenzie wawili walikimbia kwa kuwa
ilikuwa rahisi kwao kuwaona polisi kwani walikuwa nje, huyu mwenzao
aliyekamatwa akiwa ndani ya kaburi,” alisema Kamanda Kidavashari. Aliwataka
watu au mtu yeyote aliye na taarifa, juu ya walipo watu hao, kutoa taarifa kwa
vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya
mashuhuda wa tukio hilo, zinaeleza kuwa mtuhumiwa alikutwa ndani ya kaburi
akiwa amemaliza kazi ya kutoa udongo.
BY: EMMY MWAIPOPO
CHANZO: HABARILEO
No comments:
Post a Comment