Na Nathaniel Limu, Singida
Watu wawili wakazi wa jimbo la
Singida Kaskazini mkoani Singida, wamefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa
hatari wa Kipindupindu unaotokana na uchafu.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi jana ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Singida, Elias Tarimo, alisema
Novemba, 26 mwaka huu, ugonjwa huo wa Kipundupindu ulibainika katika vijiji vya
Merya na Msange jimbo la Singida kaskazini.
Hata hivyo, alisema kuwa ilichukua
muda mrefu mno mamlaka zinazohusika kutoa taarifa ya ugonjwa huo, kitendo
kilichochangia idadi ya wagonjwa kuongezeka na kufikia 30.
“Urasimu huu umesababisha hatua
stahiki za kudhibiti ugonjwa huu, kuchelewa kuchukuliwa na hivyo kuchangia
wananchi wawili kupoteza maisha. Kwa sasa tumebakiwa na wagonjwa sita kambi ya
Merya na Msange wapo watatu,” alisema Tarimo.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema baada
ya kupata taarifa hizo kwa kuchelewa, hawakulala walipiga kampeni ya nguvu
kuhimiza usafi wa mazingira, matumizi bora ya vyoo na kuchemsha maji kwa ajili
ya matumizi ya nyumbani.
“Aidha, wataalam walipima maji ya
visima 14 yanayotumiwa na wananchi wa vijiji hivyo, na 12 kubainika vina vidudu
vinavyochangia ugonjwa wa kipindu pindu. Baada ya kugundua hivyo, tumepiga
marufuku maji ya visima hivyo kutumika,” alisema.
Akifafanua, alisema wamewaelekeza
wananchi kutumia maji ya bomba na wamechukua mashine kubwa ya kupampu maji
kutoka kijiji cha Sagara.
“Mashine hii tumeisimika na
itasambaza maji ya bomba katika vijiji hivyo vya Msange na Merya. Hatujaishia
hapo, tunaendelea kuwahimiza wananchi kutumia vidoge vya waterguird kwa ajili
ya kutibu maji yawe safi na salama. Vile vile tanawahimiza kutumia vyoo na
kuacha tabia ya kujisaidia ovyo kwenye vichaka,” alisema.
Katika hatua nyingine, Tarimo
alisema kuwa baada ya kufanya kampeni ya kuhimza usafi, mwananchi yoyote
atakayeugua Kipindupindu, atatibiwa na akipona, mara moja atafikishwa
mahakamani, kujibu tuhuma ya kutaka kujiuawa kwa makusudi.
Wakati huo huo, katika kuchukua
hatua kudhibiti Kipindupindu, Manispaa ya Singida imechukua hatua mbalimbali,
ikiwemo ya kupiga marufuku wafanyabiashara wa matunda, kumenya matunda.
Imeagizwa kuwa matunda yote yaliwe nyumbani baada ya kuoshwa vizuri kwa maji.
Pia kila kaya imeagizwa kutumia
vyoo bora na kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula chakula na baada ya kutoka
chooni.
Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bravo
Kizito Lyapembile, amesema mtu ye yote akikamatwa kwa kuchafua mazingira,
atatozwa faini kati ya shilingi 30,000 na 300,000.
No comments:
Post a Comment