Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema haitaoongeza siku za kufanya
uhakiki wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) jijini Dar es Salaam baada
ya muda kumalizika leo, na hivyo wote watakaokuwa hawajahakikiwa watafutiwa
namba zao na watatakiwa kuomba upya.
Kwa
mara ya kwanza TRA ilipanga kufanya uhakiki wa TIN kwa siku 60 kati ya Agosti
na Oktoba lakini baada ya kujitokeza watu wengi tarehe ya mwisho iliongezwa
hadi Novemba na mara ya tatu ilisogezwa hadi Januari 31. Lengo la uhakiki huo
ni kuondokana na mfumo wa kizamani wa usajili wa namba hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi (TRA), Richard Kayombo, alisema kutokana na idadi kubwa ya watu
waliokuwa wanahitaji kuhakikiwa namba, mamlaka iliamua kusogeza mbele muda wa
kutoa huduma hiyo pamoja na kufungua vituo vya kutoa huduma ambako watumishi
walifanya kazi hiyo hadi Jumamosi na Jumapili kuwapa nafasi wafanyakazi.
Alisema madhara kwa watakaofutiwa
TIN ni makubwa kwani wafanyabiashara na madereva wa magari leseni zao zitakuwa
batili na watachukuliwa hatua kwa kosa la kufanya biashara bila kuwa na namba
ya utambulisho.
“Wale wote ambao watakuwa
hawajahakikiwa watafutiwa namba zao za TIN, itawalazimu kuomba upya ingawa
kuomba kwao upya hakutafuta madeni yao ya nyuma,” alisisitiza Kayombo.
Mmoja wa watu waliokwenda kuhakiki
namba zao kituo cha Mwenge, Abdul Namwelesi alikosoa utaratibu huo akipendekeza
uhakiki ungekuwa endelevu badala ya kuweka muda maalumu kutokana na ugumu wa
watu wote kuhakikiwa kwa wakati mmoja.
BY: Emmy Mwaipopo
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment