Vigogo watatu ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Ugavi wa Umeme
Tanzania (Tanesco), makao makuu Dar es Salaam, wameshushwa vyeo huku mmoja
akiamua kuacha kazi mwenyewe.
Hatua
hiyo imekuja siku nne tangu Rais Dk. John Magufuli atengue uteuzi wa aliyekuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Mramba alitenguliwa uteuzi wake
siku chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),
kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5
kutoka 18 waliyoomba.
Wakurugenzi hao wamesimamishwa jana
kupisha uchunguzi, huku chanzo cha kusimamishwa kwao kikiwa hakijaelezwa.
Taarifa kutoka ndani ya Tanesco
ambayo ilithibitishwa na Kaimu Mkurugenzi mpya wa shirika hilo, Dk. Tito
Mwinuka kwa simu jana, ilieleza kusimamishwa kwa vigogo hao ambao walikuwa
wasaidizi wa karibu wa Mramba katika utendaji.
“Ni kweli wamesimamishwa, lakini
kwa kuwa sikuwa ofisini ngoja niisome vizuri taarifa iliyopo mezani kisha
niwatumie taarifa iliyokuwa sahihi kuhusiana na hilo.
“Hapa nilipo nipo ofisini na ofisa
habari wangu (hakumtaja jina) tunaandaa taarifa ya pamoja, kwa maana kila mmoja
anapiga simu kutaka taarifa, hivyo siwezi kuzitoa nusu nusu,’’ alisema Dk.
Mwinuka.
Hata hivyo, hadi tunakwenda
mitamboni taarifa hiyo ilikuwa bado haijatumwa na alipopigiwa tena simu Dk.
Mwinuka hakupokea.
Taarifa zinaeleza kwamba
wakurugenzi watatu wameshushwa vyeo na kuhamishiwa katika Chuo cha Mafunzo cha
Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi wake.
Source: Mtanzania
No comments:
Post a Comment