WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini kuacha kutoa fedha
taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.
Badala yake amewataka waandae mfumo
maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za mfuko wa Jimbo ambazo ni
maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za maendeleo jimboni.
Ametoa kauli hiyo jana mchana
(Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa
wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo Manispaa
ya Songea.
“Nimepata taarifa kuwa fedha za
maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana. Msiwape fedha mkononi,
bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na matumizi ya
aina hiyo, mwisho wake ni jana,” alisisitiza.
“Fedha za mfuko wa Jimbo ni za
Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri na yeye
anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni miradi
ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa imekwishaidhinishwa na vikao
husika,” aliongeza.
Alisema makusanyo ya fedha
yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha hizo
zinavyotumiwa.
“Lazima tukishakusanya tuangalie
tumepata kiasi gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila
diwani. Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye miradi
ya maendeleo,” alisisitiza.
Alisema kuna baadhi ya watu
wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia kutumia fedha
hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building).
“Hii si sahihi na jana nimepiga
marufuku posho za aina hii pamoja na fedha za vitafunwa kwa sababu zinaishia
kwa wakubwa wachache na waliozikusanya hawapati chochote,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa
mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu aliwataka waangalie baadhi ya makampuni
ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini wanatumia software
ambazo zinawanufaisha na wao pia.
“Tumieni watu wenu wa TEHAMA
kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile mashine siyo
waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna mianya ya wizi.
Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia kwenye akaunti
za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu wanayoijua wao. Ukiangalia
unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia unaibiwa. Jaribuni kuchunguza na
mjiridhishe na hizo software zao,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI
MKUU
No comments:
Post a Comment