Andrew Puzder, aliyekuwa ameteuliwa
na Rais wa Marekani Donald Trump kuwa waziri wa masuala ya wafanyakazi,
amejiondoa muda mfupi kabla yake kuhojiwa na wabunge.
Puzder alipoteza uungwaji mkono wa maseneta kadha wa chama cha
Republican baada yake kukiri kwamba alimwajiri mhamiaji aliyeingia Marekani
kinyume cha sheria kuwa mjakazi.
Bilionea huyo pia amekosolewa kwa matamshi yake kuhusu wanawake na
wafanyakazi katika migahawa yake.
Yeye sasa anakuwa mtu wa kwanza miongoni mwa waliopendekezwa na
Trump kuwa waziri kukosa kuidhinishwa.
Talaka yake na mkewe mwaka 1980, ambayo ilikumbwa na mvutano
mkubwa, pia imemwathiri.
Majuzi, ilibainika kwamba mke wake wa zamani, Lisa Fierstein,
alishiriki kama mwathiriwa wa udhalilishaji kwenye ndoa katika kipindi cha
Oprah Winfrey mwaka 1990 ambacho kilifahamika kwa jina High Class Battered
Women (Wanawake wa tabaka la juu wanaopigwa na waume zao).
Walitalikiana mwaka 1987, lakini baadaye aliondoa tuhuma za
udhalilishaji dhidi ya Puzder wakati wa makubaliano kuhusu nani angewatunza
watoto.
No comments:
Post a Comment