Wapigakura wanne wa Jimbo la Bunda
waliofungua shauri kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita wameendelea
kumng’ang’ania mbunge wa jimbo hilo, Ester Bulaya kwa kukata rufaa kupinga
uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupa maombi yao.
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya
Mwanza, Francis Kabwe alisema jana kuwa rufaa ya wapigakura hao, Magambo
Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila iliyosajiliwa kwa
namba 199 ya mwaka 2016, itasikilizwa mfululizo kuanzia Februari 20.
Alisema rufaa hiyo itasikilizwa
jijini Mwanza na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Salim Mbarouk,
Augustine Mwarija na Shabani Lila.
Katika maombi ya msingi
waliyofungua Mahakama Kuu, wapigakura hao wanaowakilishwa na Wakili Constantine
Mutalemwa, wanaiomba Mahakama kutengua ushindi wa Bulaya dhidi ya aliyekuwa
mgombea wa CCM, Stephen Wasira kwa madai kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka 2015
haukuwa huru na wa haki.
Pamoja na madai mengine, Masato na
wenzake wanadai kuwa mchakato wa kampeni, upigaji kura na utangazaji wa matokeo
uligubikwa na ukiukwaji wa sheria na utaratibu wa uchaguzi, vikiwamo vitendo
vya rushwa, msimamizi wa uchaguzi kumnyima haki Wasira kwa kukataa ombi lake la
kura kuhesabiwa upya.
Hoja nyingine ni msimamizi wa
uchaguzi kutangaza matokeo bila Wasira kuwapo ukumbini na kuchanganya tarakimu
za idadi ya wapigakura walioshiriki uchaguzi.
Novemba 17, mwaka jana, Jaji Noel
Chocha wa Mahakama Kuu alimtangaza Bulaya kuwa mshindi halali wa uchaguzi huo
baada ya kutupilia mbali maombi ya wapigakura hao.
No comments:
Post a Comment