Hali ya ulinzi imeimarishwa katika
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikolazwa mfanyabiashara Yusuf Manji
baada ya kuugua ghafla akiwa polisi alikokuwa akihojiwa.
Manji aliyekuwa akihojiwa katika
Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapa alipelekwa hospitalini hapo juzi jioni akiwa
ndani ya gari la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser lenye nembo ya Shirika la
Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) huku gari lake aina ya Range
Rover likifuata kwa nyuma.
Askari wenye sare na wengine wakiwa
na mavazi ya kiraia nje ya wodi aliyolazwa mwenyekiti huyo wa klabu maarufu
nchini ya Yanga walionekana wakiimarisha ulinzi.
Ilipofika saa 4:13 asubuhi
mfanyabiashara huyo alitoka kwenye chumba hicho na kuongozwa kuelekea upande
mwingine wa jengo hilo.
Akiwa amevalia nguo za wagonjwa
zenye rangi ya kijani, Manji alitembea taratibu kuelekea upande aliokuwa
akielekezwa.
Alipoulizwa kuhusu uwapo wa Manji
hospitalini hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema
hawezi kuzungumzia taarifa za mgonjwa.
Februari 8, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda alitoa orodha ya watu 65, akiwamo Manji ambao aliwataka
wafike Polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu masuala ya dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment