Polisi mkoani Ruvuma
inamshikilia Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kitanda wilayani Namtumbo,
Gislary Tweve kwa tuhuma za kumshambulia mkulima na mkazi wa Kijiji cha
Kitanda, Adolf Nyoni (34) baada ya kukataa kulipa kinywaji aina ya Konyagi, kilichokuwa
katika kifungashio cha plastiki (kiroba) alichokunywa katika duka la kanisa
hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zuberi
Mwombeji alisema padri huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 10, mwaka huu, saa
mbili usiku katika duka la Parokia ya Kitanda.
Kamanda Mwombeji alisema Padri
Tweve alimpiga Nyoni kichwa na makofi, kisha kumrukisha kichura kwa kile
kinachodaiwa kukataa kulipa pombe hiyo ambayo imekatazwa kisheria, lakini duka
hilo bado limekaidi na kuendelea kuuza pombe hiyo.
Alisema Polisi inaendelea na
uchunguzi kuhusu tukio hilo na mara utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa
mahakamani.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa rai
kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma, kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa
mbalimbali katika vyombo vya dola, badala ya kujichukulia sheria mkononi na
kuachana na biashara iliyopigwa marufuku ya pombe kali zilizofungwa kwenye
vifungashio vya plastiki.
Kuanzia Machi mosi, mwaka huu,
serikali imepiga marufuku utengenezaji, usambazaji, uuzaji na unywaji wa pombe
zilizowekwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kwa jina la viroba, na
kuibainisha kuwa itatoa adhabu zikiwemo faini za hadi Sh milioni tano, kifungo
jela au vyote kwa pamoja, kwa watakaokiuka marufuku hiyo.
Serikali imechukua hatua hiyo baada
ya kubainika kwamba mbali ya kuikosesha mapato serikali yanayofikia Sh bilioni
600 kwa mwaka, pombe hizo za kwenye viroba zimekuwa zikitumiwa isivyo kutokana
na ufungashaji wake wa kirahisi.
No comments:
Post a Comment