Figisufisu
na ugomvi kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda na
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima (GCTC), Josephat Mathias Gwajima,
zimepamba moto na joto lake linapanda na kushuka kila kukicha.
CHANZO CHA
UGOMVI WA MAKONDA NA GWAJIMA
Nyuma ya
ugomvi huo unaotajwa kuwa wa kihistoria huku mmoja akimwaga mboga na mwingine
anamwaga ugali, duru za kisiasa zinadai kwamba, chanzo cha yote hayo ni Ubunge
wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Uwazi limedokezwa.
Jimbo la
Misungwi kwa sasa linaongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Charles Muhangwa Kitwanga.
KITWANGA NA
UWAZI
Akizungumza
na Uwazi katika mahojiano maalum na kutoa la moyoni juu ya sakata hilo mwishoni
mwa wiki iliyopita, Kitwanga aliwavaa wawili hao akiwashangaa kusikia kwamba
wanalitaka jimbo lake hilo.
Kitwanga
alikiri kuwa, amezisikia habari hizo lakini kinachomshangaza ni kwamba, ni
mapema mno kwani ni mwaka wa pili tu, tangu uchaguzi ulipomalizika mwaka 2015
na uchaguzi mwingine upo mbali kwani ni hadi mwaka 2020.
KITWANGA
AFUNGUKA
“Taarifa
hizo nimezisikia lakini kinachonishangaza ndiyo kwanza tumetoka kwenye uchaguzi
na uchaguzi mwingine bado sana.
“Kwani
tayari umeshafika muda wa kugombea?
Wameshapitishwa
na vyama vyao?
Ninachojua
ni kwamba, sisi tumemaliza uchaguzi na sasa tunafanya kazi, mimi natekeleza
ilani ya chama changu (CCM).
WAACHE
KUVURUGA WANANCHI
“Kama
wanagombana na wao wanataka jimbo langu, wasubiri muda utakapofika tufanye
kampeni na siyo kuvuruga wananchi wangu. Katika taratibu zetu ndani ya chama
ziko tofauti sana.
“ Najua
Gwajima ni mwanachama wa Chadema na Makonda anaiami n i CCM, wao wana taratibu
zao lakini wasivuruge wananchi wangu ninaowatumikia, wao waendelee na hayo
mambo yao.
WANAKARIBISHWA
ULINGONI
“Hata hivyo,
simzuii mtu kugombea katika jimbo langu, wanakaribishwa ulingoni lakini wafuate
taratibu za vyama vyao muda utakapofika tutajua, huu ni muda wa kuchapa kazi
kama ilivyo kauli mbiu ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu na ndicho
ninachokifanya kwa wananchi wangu na si vingine na wala sitaki kuwaingilia
kwenye huo ugomvi wao,” alisema Kitwanga.
YATOKANAYO
Katika
uchunguzi wake, Uwazi lilidokezwa na vyanzo vyake kuwa, Makonda anatajwa kutaka
ubunge wa jimbo hilo ili kupandisha kiwango chake cha kisiasa na hata kufikia
ngazi ya uwaziri baada ya 2020.
Hata hivyo,
suala la wawili hao kuhusishwa na jimbo hilo iliwahi kuelezwa na Askofu Gwajima
siku chache baada ya kutajwa na Makonda kwenye kuhusika na mambo ya dawa za
kulevya hivyo kudai kuwa ni vita ya kisiasa.
Gwajima
anayetoka kijiji kimoja na Makonda cha Koromije jimboni Misungwi alikaririwa
kanisani kwake akisema kuwa zipo taarifa za Makonda kumsakama kwa sababu
anadhani na yeye (Gwajima) analitaka jimbo hilo.
“Nilipata
msiba nyumbani Koromije nilikozaliwa, kwa kuwa nilitoka muda mrefu huko hivyo
nilikwenda msibani kwa helikopta.
“Kule kuna
shangazi yangu, nilitua kwa ndugu wengine na kama unavyojua helikopta ikitua
kijijini, lazima watu waje wengi kuitazama.
GWAJIMA NA
KITWANGA
“Nilipoondoka,
watu wakabaki wakiita Gwajima… Gwajima. Baada ya wiki tatu, nne, kaka yangu
ambaye ni mtoto wa shangazi alifariki dunia, nikaona safari hii nikiwa
ninakwenda kule nimpigie Mbunge wa Misungwi (Kitwanga), nikamweleza kuwa
nitakwenda kule tena kwenye jimbo lako, naomba ukiwa na nafasi twende wote…
sitaki unione ninakwenda kwa madhumuni ya kisiasa.
“Nilipokwenda,
Kitwanga alikuwa bize, akasema nenda na katibu wangu, nikamchukua na mbunge
mwingine wa zamani wa jimbo hilo nikasema twende wote ili wasifikiri kwamba
Gwajima anataka kufanya kitu.
“Nikatua na
helikopta pale msibani, si unajua tena, wakaniambia ongea lakini sikuhutubia
lolote. Nikakaa na mapailoti wetu na baada ya msiba nikaondoka.
GWAJIMA NA
MAKONDA
“Sasa
baadaye ndiyo watu wakasema yule kiumbe (Makonda) alikuwa anataka lile jimbo,
ulipokwenda wewe alihisi unataka kulichukua mwaka 2020, nikasema angeniuliza,
kwa mimi siwezi kuwa mbunge, nikiwa mbunge ni kujishusha, mimi ni mtumishi wa
Bwana ambaye ni zaidi ya mbunge, waziri na rais, siwezi kugombea urais uwaziri
au ubunge, nitakuwa nimejishusha, mimi ni mtumishi wa Mungu aliye hai.
“Kwa hiyo
Makonda alidanganyika na kujikuta akinitaja kwenye madawa ya kulevya akijua
atakuwa amenimaliza kwa wananchi bila kujua sina ndoto hiyo,” alidai Gwajima
lakini Makonda yeye hajawahi kulizungumzia hilo.
Jumapili
iliyopita Uwazi lilimtafuta Makonda ili kusikia upande wake lakini simu yake
iliita bila kupokelewa.
KINACHOENDELEA
Jumapili
iliyopita Gwajima aliendelea kutumia kanisa lake kumshambulia Makonda juu ya
suala ya vyeti feki huku akiweka hadharani ‘document’ aliyodai ni cheti cha
kidato cha nne cha Makoda cha Shule ya Sekondari ya Pamba iliyopo Mwanza.
Hata hivyo,
Makonda wiki iliyopita akiwa na watu waliokuwa wakitumia madawa ya kulevya
alizungumzia elimu yake kwa kujigamba kwamba akiwa rais wa wanafunzi wa vyuo
vikuu alifanya makubwa na hakuzungumza chochote kuhusu vyeti feki anavyodai
Askofu Gwajima.
No comments:
Post a Comment