Idadi kubwa
ya wakazi wa wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro wanajulikana kwa ukulima hasa
wa zao la mpunga na muwa kwa ajili ya kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.
Hata hivyo,
katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wakulima hawa walianza kukata tamaa ya
ukulima huku wengine wakijaribu kufanya shughuli mbadala kama vile kujiingiza
katika biashara ndogo ndogo. Hii ni baada ya mbegu za miwa walizokuwa wakitumia
kupoteza ubora wake, na matokeo yake kushindwa kustahamili mabadiliko ya tabia
nchi na hatimae kuvamiwa na magonjwa. Masoud Mohamed Mshame ambae ni mkulima wa
miwa kutoka wilayani humo anakiri kwamba kila mwaka, mavuno yalikuwa
yakipungua.
"Kulingana
na mabadiliko ya hali ya hewa, mwaka jana na mwaka juzi, tulivuna mapato ya
chini tofauti na kipato tulichokuwa tunategemea siku za nyuma. Kwa miaka mitatu
iliyopita, tulikuwa tunavuna kuanzia tani 30. Ilipofika mwaka jana, tulivuna
hadi tani 20 na chini ya hapo," amesema Masoud.
Hivi sasa
hali imeanza kubadilika. Baadhi ya wakulima wanaonekana kujawa na hamasa na
matumaini ya kufanya vizuri katika kilimo. Hii ni baada ya kufikiwa na mradi wa
endelevu maarufu kama SUSTAIN ambao umejikita zaidi katika kuzalisha mbegu za
miwa ambazo baada ya kufanyiwa utafiti na Kituo cha Utafiti wa Miwa Kibaha,
imethibitika kwamba zina ubora na uwezo wa kustahamili ukame.
Mradi huu
una wadau mbalimbali, miongoni mwao ni Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Afrika
ukishirikiana na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, pamoja na Kituo cha Utafiti
wa Miwa Kibaha.
Mpaka sasa
takriban wakulima elfu moja, huku asilimia arobaini kati yao wakiwa ni
wanawake, tayari wapo katika mpango wa mashamba darasa ya kilimo bora cha miwa
ambayo yamewapa muongozo katika kuboresha kilimo hicho na kutunza miwa
shambani, hali inayotarajiwa kuongeza mavuno na kufikia hadi tani 70 za miwa
kwa hekta tofauti. Hii ni tofauti na awali ambapo baadhi ya wakulima wanakiri
kupata kiwango kidogo.
Mbegu bora
hupatikana kwenye mashamba makubwa ya kiwanda cha Kilombero, ambapo kabla ya
kupandwa, hupitia teknolojia maalum ya kuchemshwa katika maji yenye dawa hadi
kufikia nyuzi joto hamsini kwa lengo la kuzuia kushambuliwa na magonjwa kama
vile Smart.
"Tunachokifanya
hapa ni kuhakikisha kwamba tunaitibu hii mbegu kabla ya kuipanda ili
kuhakikisha kwamba iko salama kutokana na wadudu na magonjwa," amefafanua
mmoja wa wataalam wa mbegu katika kiwanda cha Sukari cha Kilombero.
Kwa mujibu
wa watafiti, iwapo vitalu vya mbegu vitahudumiwa kitaalamu shambani, basi kuna
uwezekano mkubwa wa kudumu hadi miaka nane mpaka kumi.
Hata hivyo,
kilimo cha miwa ni biashara ambayo inahitaji maji mengi na mbolea ya kutosha.
Pastor Magingi ambae ni meneja mradi-Sustain anasema wameamua kujikita zaidi
katika kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, ili wawe na kipato cha uhakika, hivyo
kupunguza uwezekano wa kuharibu misitu inayowazunguka.
Tanzania ina
viwanda vikuu vinne vya sukari, na kumekuwa na mpango wa kuongeza uzalishaji
sukari kufikia tani laki tatu kabla ya mwaka 2020. Lakini, wakati huo huo,
wachambuzi wa mambo, wanahisi kabla ya lengo hilo kuweza kufikiwa, baadhi ya
changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la muwa, zinahitaji kufanyiwa kazi
ili kuongeza uzalishaji.
No comments:
Post a Comment