
Na: Frank
Shija – MAELEZO.
TPDC kwa kushirikiana na Sekta binafsi wanatarjia kutekeleza
miradi mbalimbali ya usambazaji wa gesi asilian katika Mikoa ya Dar es Salaam,
Pwani, Lindi, Mtwara na baadhi ya mikoa mingine itakayoidhinishwa.
Hayo yamebainishwa na Kiamu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi
Kapuulya Musomba wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake
jana Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Musomba alisema kuwa miradi hiyo imeanza kwa kupitia
upya taarifa ya awali ya upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa mtandao wa
bomba la kusambazia gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo mnamo
mwezi machi 22, 2017 TPDC ilikaribisha jumla ya makampuni 9 ambayo yalikidhi
vigezo vya kimanunuzi kwa ajili ya kazi hiyo.
“Napenda kuutaarifu umma kuwa TPDC inatarajia kutekeleza miradi
mbaimbali ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Bagamoyo
na Mkuranga Mkoani Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na baadhi ya mikoa mingine,” alisema Mhandisi Muyomba.
Aliongeza kuwa lengo la kupitia upya taarifa za awali ni
kuboresha zaidi taarifa za kifedha, mahitaji ya kiufundi na utambuzi wa njia za
kupitisha bomba na ugawaji wa kanda za usambazaji.
Aidha alisema kuwa ili kuharakisha usambazaji wa gesi, TPDC
inakaribisha na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uendelezaji wa
miundombinu itakayowezesha usambazaji wa gesi asilia katika Jiji la Dar es
Salaam mara tu mapitio ya upembuzi yakinifu utakapomalizika.
Mtandao huo unakadiriwa kuwa na urefu wa takribani kilomita 65
ambao utahudumia, kwa kuanzia, nyumba 30,000, viwanda na vituo vya kushindilia
gesi asilia pamoja na vituo vya kujazia gesi hiyo.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema
kuwa hadi sasa TPDC imefanikiwa kukiunganisha na mtandao wa gesi asilia Kiwanda
kimoja cha kutengeneza Vigae cha Goodwill kilichopo Mkuranga, Mkoani Pwani huku
likiendelea na majadiliano na viwanda vingine vitatu kwa ajili ya kuunganishwa
na mtandao huo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 TPDC inatambuliwa
kuwa Shirika rasmi la taifa linalojiendesha kibiashara, ambapo sheria hii
inaipa mamlaka TPDC kuruhusu makampuni mbalimbali kuendesha shughuli za sekta,
zitakazokuwa zainadhibitiwa kwa utaratibu maalum chini ya usimamizi wa Mdhibiti
anayetoa leseni.
No comments:
Post a Comment