Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister
Marco (54) amepandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu
ya kuishi na kufanya kazi nchini bila kuwa na kibali.
Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay alimemsomea
mashtaka hayo leo Jumatano kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
Akisoma hati ya mashtaka, Mlay alidai kuwa Mei 19,
2017 huko Kinondoni katika ofisi ya uhamiaji, Marco akiwa raia wa
Burundi alikutwa nchini bila kuwa na kibali cha kumuwezesha kuishi.
Marco katika shtaka la pili amedaiwa kuwa siku hiyo alikutwa
akifanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila ya kuwa na kibali
kinachomruhusu kufanya kazi hapa nchini.
Katika shtaka la tatu, Mlay alidai kuwa, Julai 6 mwaka 2011
katika ofisi ya Uhamiaji ya Dar es Salaam iliyopo Wilaya ya Ilala, mshtakiwa
huyo akiwa raia wa Burundi alitoa taarifa za uongo kuhusu maelezo yake binafsi
wakati akijaza fomu ya kuomba hati ya kusafiria namba CT (5)(Ai).
Wakili Mlay alisema kitendo hicho cha kutoa taarifa za uongo
kilimuwezesha Marco kupata hati ya kusafiria ya Tanzania yenye namba AB 474856
huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikana na upande wa mashtaka
ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao
kila mmoja atasaini bondi ya Sh 20 milioni na alikamilisha. Kesi imeahirishwa
hadi Juni 21, 2017 kwa ajili ya kutajwa.
No comments:
Post a Comment