Mahakama Kuu kanda ya Mbeya, kwa kusaidiwa na ushahidi wa
baba mzazi wa mshitakiwa, imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Geoffrey Sichizya
(27) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumua babu yake ili achukue ng’ombe
wake tisa.
Akisoma hukumu hiyo kwenye Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe
jana, Jaji wa Mahakama Kuu Atuganile Ngwala alisema baada ya kusikiliza
ushahidi wa pande zote mbili ameridhika pasipo kuacha shaka kuwa mshitakiwa
alimuua babu yake Labson Sichizya kwa kukusudia.
Alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na Meas Sichezya
ambaye ni baba mzazi wa mshitakiwa huyo, pamoja na Mashaka Sichizya ambaye ni
ndugu wa damu, ambao kwa pamoja walimkamata siku ya tukio wakiwa na viongozi wa
vijiji na kumpeleka polisi.
Jaji Ngwala alisema Geofrey kwenye maelezo yake kwa mlinzi wa
amani alidai kuwa alimuua babu yake ili achukue ng’ombe tisa waliokuwa
wanamilikiwa na babu huyo.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Ofmedy
Mtenga kwamba mshitakiwa alimkaba koo babu yake Sichizya hadi kufa Novemba 19,
2012 saa 2:00 asubuhi katika kijiji cha Sakamwela, wilaya ya Mbozi mkoani
Songwe.
Aliendelea kusema kuwa mshitakiwa huyo baada ya kumuua babu yake
huyo kwa kumkaba koo na kufariki, alimfunga na kamba ya chandarua shingoni na
kumning’niza kwenye mti nyuma ya nyumba yake ili ionekane kama marehemu
alijinyonga.
Mshitakiwa huyo alikuwa akitetewa na wakili Kamru Habibu, ambaye
baada ya hukumu kutolewa hakuwa na hoja yoyote mbele ya mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment