Jafo aziagiza Halmashauri zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kurejesha mikopo yao - OREST NGOWI

Breaking

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Friday 13 October 2017

Jafo aziagiza Halmashauri zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kurejesha mikopo yao

Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amezitaka Halmashauri zote zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kurejesha madeni yao kabla ya Desemba 30 mwaka huu.

Jafo ametoa agizo hilo  jana Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu marejesho ya mikopo katika bodi hiyo kutoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 9.7 hadi Septemba 30, 2017 kwa Halmashauri 54. Hadi Septemba 30, 2017 jumla ya shilingi 6.57 zilirejeshwa,” alisema Jafo.

Aliendelea kwa kusema kuwa halmashauri nyingi zimejitahidi katika kurejesha mikopo waliyochukua lakini kuna Halmashauri 9 zimeonyesha usugu uliopitiliza katika kurejesha mikopo hiyo, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 2 hazijarejeshwa kutoka katika Halmashauri hizo.

Jafo amezitaja Halmashauri zilizoonyesha usugu kuwa ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Mbeya, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Singida na Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Karatu, Pangani, Igunga, Mbinga, Mji Mbinga na Kongwa.

Aidha amesema kuwa , kitendo cha usugu katika urejeshaji wa mikopo kinanyima fursa kwa Halmashauri nyingine kupata mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hivyo basi, Waziri Jafo amemtaka Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo kufanya ufuatiliaji ili wadaiwa wote waweze kurejesha mikopo yao na wadaiwa sugu kurejesha mikopo kabla ya Desemba 30, mwaka huu.

Hata hivyo Jafo ameitaka Bodi hiyo kuangalia utaratibu wa kupitisha mikopo inayolenga ujenzi wa viwanda na uwekezaji katika Halmashauri ili kukuza ajira na uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa Richard Mfugale amesema kuwa bodi itatekeleza agizo la Waziri na tayari imeshafanya mawasiliano na halmashauri zinazodaiwa kuona vyanzo vya mapato watakavyoviachia kwa ajili ya kulipa madeni yao.

Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ilianzishwa kwa lengo la kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kupata mikopo ili kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo na utoaji huduma za jamii katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here