Vyama tisa vya siasa kati ya 22
vyenye usajili wa kudumu vipo hatarini kufutwa kutokana na kushindwa kukidhi
vigezo na matakwa ya kisheria yaliyoviwezesha kupata usajili wa kudumu.
Hatua ya kufutwa vyama hivyo,
vikiwamo baadhi visivyo na ofisi za kudumu (vyama vya mfukoni) itafikiwa ikiwa
vitashindwa kujieleza kutokana na makosa ambayo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa imebaini katika ukaguzi uliofanyika hivi karibuni Bara na Visiwani.
Jukumu kubwa la Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa ni kusimamia, kuboresha, kuendeleza na kudumisha demokrasia ya
vyama vingi hapa nchini majukumu ambayo yanatokana na Sheria ya Vyama vya Siasa
Na. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi Na. 7 ya mwaka 2010.
Majukumu mengine ya ofisi ya
msajili ni kusajili vyama vya siasa na kuvifuta vyama ambavyo havikidhi matakwa
ya sheria hiyo na kusimamia ugawaji wa ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa
kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza ofisini kwake
jana, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema uhakiki
uliofanywa na ofisi yake katika vyama hivyo upande wa Bara na Visiwani umebaini
kasoro nyingi zikiwamo za ukiukaji wa masharti ya usajili.
“Katika uhakiki uliofanywa na
ofisi yangu tumebaini kasoro mbalimbali ambazo kwa mujibu wa sheria ya
vyama vya siasa ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyoangaliwa ili chama kiwe na
sifa ya kusajiliwa,”alisema.
“Kasoro tulizozibaini ni nyingi na
baadhi ya vyama kutokana na mapungufu waliyo nayo huhitaji kutoa nafasi
tena….unaweza kuvifuta hapohapo.”
Msajili hakutaka kutaja majina ya
vyama hivyo ambavyo tayari vimeandikiwa barua lakini alitaja makosa kuwa baadhi
havina ofisi za kudumu Tanzania Bara na Visiwani au upande mmoja na vingine
havina anuani ya posta.
“Unakuta chama fulani kina ofisi
labda Zanzibar lakini hakina ofisi Bara,”alisema Jaji Mutungi. Alisema vyama
vingine havina viongozi wa kitafa kutoka pande mbili za Muungano na pia havina
bodi ya wadhamini iliyosajiliwa kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
(Rita) kama sheria inavyohitaji.
Katika ukaguzi huo, Msajili
alibaini pia kasoro nyingine kuwa ni kukosekana kwa orodha ya wanachama wa
chama husika jambo alilosema nalo ni muhimu kila chama kuwa na orodha ya idadi
ya wanachama wake.
Vilevile, baadhi ya vyama hivyo
vimeshindwa kuonyesha akaunti ya fedha ya chama hali inayotia shaka namna
vinavyojiendesha.
No comments:
Post a Comment