Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu
Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutuhumu baadhi ya viongozi wake
waliosimamishwa uanachama kupanga njama za utekaji viongozi wa chama hicho,
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikiliwa wanachama wa CUF
22 kwa tuhuma za kupanga njama za kufanya fujo na kuchoma mali za ofisi za
chama hicho.
Ikumbukwe kuwa, Septemba 16,2016
CUF kupitia Kurugenzi yake ya Habari na Uenezi ilitoa taarifa ya jaribio la
utekaji wa Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF, Joran Bashange ambapo chama hicho
kiliwatuhumu Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya na Profesa Ibrahim Lipumba kuwa
walinzi wao walijaribu kufanya tukio hilo.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro jana alisema wanachama hao walikamatwa na
zana za kufanyia uhalifu yakiwemo mapanga, Jambia, visu na chupa za kupulizia
10 zikiwa kwenye boksi lenye maandishi ya lugha ya kichina.
Watuhumiwa hao walikamatwa Septemba
25,2016 maeneo ya Mwananyamala katika gari ya abiria ambayo ruti yake inapitia
njia ya Buguruni-Mwananyamala.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa
hao walikamatwa baada ya askari kupata taarifa kwamba wamekuja Dar es Salaam
wakitokea visiwani Unguja kutoka katika matawi mbalimbali ya chama hicho kwa
lengo la kufanya fujo.
Aidha, Sirro alisema baada ya
watuhumiwa hao kuhojiwa, walieleza kuwa wamekuja kutokana na maelekezo ya
kiongozi wa CUF Nassoro Ahmad Mazrui ambaye ni Naibu Katibu mkuu wa chama hicho
aliyewataka kuungana na walinzi wenzao waliopo katika makao makuu ya chama
hicho yaliyopo Buguruni.
Hata hivyo, baada ya taarifa za
watuhumiwa hao kukamatwa kuenea katika mitandao ya kijamii, baadhi ya watu
walimhusisha aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa CUF kwa muda Julias
Mtatiro kuhusika katika mipango ya njama hizo.
Lakini Kamanda Sirro alieleza kuwa
hadi sasa hajapokea taarifa hiyo ya kuhusika kwa Mtatiro na kwamba taarifa hizo
si za kweli.
No comments:
Post a Comment