MAAZIMIO NA
MAAMUZI YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LILILOKUTANA KWENYE MAKAO MAKUU YA
CHAMA, MJINI ZANZIBAR
TAREHE 27
SEPTEMBA, 2016
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) limekutana leo, Jumanne,
tarehe 27 Septemba, 2016 katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya
Chama, mjini Zanzibar na ambacho kiliitishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa
mujibu wa Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014), Ibara ya 80 (1). Wajumbe 43
kati ya wajumbe 53 wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa walihudhuria kikao hicho.
Agenda tatu zilizotayarishwa na
kuwasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa zilijadiliwa na kufanyiwa maamuzi
ambazo ni:
1. Kujadili barua ya Msajili wa
Vyama vya Siasa ya tarehe 23/09/2016;
2. Kupokea na kujadili mashtaka
dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba kutokana na hujuma alizozifanya tarehe
24/09/2016 Afisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam;
3. Kumjadili na Kumhoji Prof.
Ibrahim Lipumba mbele ya kikao na kumchukulia hatua za kinidhamu.
Baada ya mjadala wa kina wa agenda
hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio na maamuzi yafuatayo:
KUHUSU BARUA YA MSAJILI WA VYAMA
VYA SIASA YA TAREHE 23/09/2016:
1. Baraza Kuu limeukataa ushauri,
msimamo na mwongozo wa Msajili wa Vyama vya Siasa alioutoa kupitia barua yake
ya tarehe 23/09/2016 kwa sababu Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties
Act, No. 5 of 1992) – Sura ya 258 haimpi mamlaka wala uwezo wowote kutoa
ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao
vya Chama na kwa kulitambua hilo ndiyo maana katika matamko yake yote
aliyoyatoa, Msajili huyo ameshindwa kutaja kifungu gani cha sheria hiyo kinampa
uwezo huo.
2. Baraza Kuu limesikitishwa sana
na kitendo cha Jaji Francis Mutungi kujishushia hadhi, kujifedhehesha na
kujivunjia heshima mbele ya macho ya jamii ndani na nje ya nchi, yeye na Ofisi
anayoiongoza kwa kuvunja sheria na kudharau maamuzi ya Mahakama Kuu ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo
katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of
Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo
aliamua kwamba:
“… I do not see anywhere in the
Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn
meetings of political parties or decisions that they make.”
Tafsiri yake ikiwa ni kwamba, “…
Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya
kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa ay maamuzi ambayo vikao hivyo
vinafanya.”
3. Baraza Kuu limemuagiza Katibu
Mkuu wa Chama kumjibu kwa maandishi na kwa kina Msajili wa Vyama vya Siasa na
kumueleza maamuzi ya Baraza hilo ambalo kikatiba ndilo lenye madaraka ya
kusimamia uendeshaji wa Chama kwamba halitambui ushauri, msimamo na mwongozo
huo na limeutupilia mbali kwa kukosa kwake mantiki, hoja na pia kukosa nguvu za
kisheria.
4. Baraza Kuu linamtanabahisha
Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na
yatakayofanywa na Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni ambacho
kilivamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam tarehe 24 Septemba, 2016 na
kupiga watu na kufanya uharibifu wa mali kutokana na tamko lake hilo ambalo
halina msingi wa kisheria.
KUHUSU MASHTAKA DHIDI YA PROF.
IBRAHIM LIPUMBA KUTOKANA NA HUJUMA ALIZOZIFANYA TAREHE 24/09/2016 AFISI KUU YA
CHAMA, BUGURUNI, DAR ES SALAAM:
1. Baraza Kuu limepokea mashtaka
dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba yaliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa
ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 108 (1) ndiyo yenye mamlaka ya
kusimamia nidhamu ya Chama katika ngazi ya Taifa na kuyawasilisha mapendekezo
yake mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
2. Baraza Kuu limeridhika kwamba
Kamati ya Utendaji ya Taifa imefuata masharti yote ya Katiba ya Chama ya 1992
(Toleo la 2014) katika kuanda mashtaka hayo kutokana na mtuhumiwa, Prof.
Ibrahim Lipumba, kuvunja Katiba ya Chama, Ibara ya 12 inayohusu ‘Wajibu wa
Mwanachama” hasa Ibara ndogo za 12 (6), 12(7) na 12(16).
KUHUSU KUMJADILI NA KUMHOJI PROF.
IBRAHIM LIPUMBA MBELE YA KIKAO NA KUMCHUKULIA HATUA ZA KINIDHAMU:
1. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa ilimfikishia mtuhumiwa, Prof.
Ibrahim Lipumba, barua ya wito (Kumb. Nam. CUFHQ/OKM/WM/2016/Vol.1/49 ya tarehe
24/09/2016) ambayo pia ilikuwa na maelezo ya tuhuma na kumtaka afike mbele ya
kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika leo, tarehe 27
Septemba, 2016, mjini Zanzibar kuja kujieleza na kujitetea kwa nini
asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba ya Chama kwa kuvunja
masharti yanayohusu “Wajibu wa Mwanachama” Ibara ya 12(6), 12(7) na 12(16).
2. Baraza Kuu limesikitishwa na
dharau iliyooneshwa na Prof. Ibrahim Lipumba dhidi ya kikao hiki ambacho ni
chombo cha juu chenye mamlaka ya kusimamia uongozi wa Chama pamoja na
kupelekewa wito wa kumtaka afike mbele yake. Kitendo hicho cha dharau
kinaonesha tu jinsi gani heshima na uaminifu wa Prof. Ibrahim Lipumba kwa Chama
ulivyoshuka.
3. Baraza Kuu limeridhika kwamba
kwa kuwa Prof. Ibrahim Lipumba akiwa mtuhumiwa alichagua mwenyewe kudharau wito
wa kufika kujieleza na kujitetea ambayo ni haki yake kama mwanachama kwa mujibu
wa Ibara ya 11(6) ya Katiba ya Chama, halikuwa na sababu ya kutoendelea
kumjadili na kuchukua hatua dhidi yake.
4. Baraza Kuu limeridhika na
mashtaka dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba kwamba kwa kitendo chake cha kuongoza
na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es
Salaam, siku ya Jumamosi, tarehe 24 Septemba, 2016 na watu hao aliowaongoza na
kuwasimamia kupiga walinzi waliokuwepo, kuvunja na kuharibu mali za Chama na
hivyo kuharibu heshima na taswira ya Chama mbele ya jamii ndani na nje kwamba
amtenda makosa kinyume na “Wajibu wa Mwanachama” kama ilivyoelezwa kwenye Ibara
ya 12(6), 12(7) na 12(16) za Katiba ya Chama.
5. Baada ya kuridhika na mashtaka
hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeamua kwa kutumia uwezo wake kwa mujibu
wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria
kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba, kuanzia tarehe ya leo, Jumanne,
tarehe 27 Septemba, 2016.
6. Kwa maamuzi haya, Baraza Kuu
linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba
kuanzia tarehe ya leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna
yoyote ile na shughuli zozote za Chama.
MWISHO:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
linawapa pole wanachama wa CUF walioathirika kutokana hatua ya Msajili
kuingilia mambo ya Chama kinyume na uwezo alio nao na pia kwa matendo ya kihuni
yaliyofanywa na Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake kuvamia Ofisi Kuu ya
Chama. Wakati huo huo, Baraza Kuu linawapongeza wanachama wote kwa kusimama
imara kukilinda Chama chao na linawahakikishia litasimamia wajibu wake wa
kikatiba kukiongoza na kukilinda Chama hiki dhidi ya njama za maadui wa ndani
na nje.
HAKI SAWA KWA WOTE
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama
Cha Wananchi)
27 Septemba, 2016
No comments:
Post a Comment