MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Bukoba
mkoani Kagera imewahukumu kifungo cha maisha watu watatu kwa makosa ya kula
njama na kuchoma makanisa mbalimbali mkoani hapa.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali,
Emmanuel Manyere alisema licha ya hukumu hiyo, bado watu hao watatu
wanakabiliwa na kesi ya kukata makoromeo na mauaji ya watu 16 ambayo inaendelea
katika Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba.
Manyere alisema watu hao watatu
ambao ni Allyu Dauda, Rashid Mzee na Ngesela Keya walifikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi, mbele ya Hakimu Mkazi wa Bukoba, Victor Biambo.
Alisema washtakiwa hao kwa pamoja
wamekutwa na hatia ya kula njama na kuchoma makanisa 16 ya madhehebu mbalimbali
mkoani hapa.
Hakimu Bigambo alisema Mahakama
imeridhishwa na ushahidi kutoka upande wa walalamikaji na kutoa adhabu ya
kifungo cha miaka saba jela kwa wote watatu kwa kosa la kula njama na kifungo
cha maisha kwa kosa la kuchoma makanisa.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Kagera Augustino Ollomi aliipongeza Mahakama kwa kutenda haki katika
kesi hiyo pamoja na kuwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa polisi
ili kukomesha vitendo kama hivyo.
Licha ya hukumu katika kesi hiyo
namba 67, bado watu hao watatu wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya watu 20 katika
maeneo mbalimbali mkoani humo inayoendelea katika Mahakama Kuu, Kanda ya
Bukoba.
No comments:
Post a Comment