Nchi ya Tanzania ni
mojawapo ya nchi inayozalisha mazao mengi kwa ajili ya biashara na pia mazao
kwa ajili ya chakula ambapo wakulima wanatumia kila njia kupata nyongeza ya
mazao shambani ili wanufaike zaidi.
Pamoja
na jitihada za serikali za kuongeza uzalishaji wa mazao hapa nchini kutoka tani
milioni 9.99 mwaka 2005/6 hadi tani milioni 16.01 mwaka 2014/15, upotevu wa
mazao baada ya kuvuna nchini bado ni tatizo kubwa. Kwa mazao ya nafaka na
mikunde inakadiriwa upotevu kwa mwaka ni asilimia 30 hadi 40.
Upotevu
wa mazao husababisha nchi kutokuwa na uhakika wa chakula na kipato cha wakulima
hupungua na hivyo huchangia pato la Taifa hushuka. Hata hivyo Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi imekuwa ikifanya
jitihada za kupunguza upotevu wa mazao nchini kupitia program na mipango
mbalimbali.
Serikali chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa
sasa (BRN) inakarabati na kujenga jumla ya ghala 275 katika wilaya 12 za Mikoa
ya nyanda za juu kusini kwa ajili ya kuhifadhia zao la mahindi. Hivyo mradi huu
wa mifuko ya PICS umekuja wakati muafaka katika kuchangia juhudi za serikali za
kudhibiti upotevu wa mazao nchini.
Chuo kikuu cha Purdue kwa kushirikiana na kiwanda cha
Pee Pee Tanzania Limited (PPTL) kilichopo Tanga – Tanzania kimeleta teknolojia
mpya “mifuko ya tabaka tatu” ijulikanayo kwa jina la PICS, mifuko iliyofanyiwa
utafiti na wataalamu kutoka taasisi ya utafiti ya ukiliguru na chuo kikuu cha
sokoine (SUA).
Utafiti uliofanywa na Profesa Rodes Makundi na Profesa
Apia Masawe wa chuo kikuu cha kilimo (SUA) uliohusisha mifuko ya PICS
umeonyesha sio tu mazao yatakuwa salama yakiwa ndani ya mifuko hiyo bali hata
wadudu wanaobangua mahindi hufa baada ya siku kadhaa bada ya kukosa hewa na
haitumii kemikali kabisa.
Wataalamu hao pia waliongeza kuwa mifuko hiyo yenye
kisalfeti nje na mifuko miwili ya nailoni nzito, matumizi yake ni lazima mazao
yawe yamekauka vizuri, ili kuzuia “wadudu wanaoharibu mazao kwa kunusa ikiwamo
panya, lakini kwa sababu mfuko huo una nailoni mbili hawatapata harufu na
waliokuwamo kwenye mazao kwa bahati mbaya hawatapata hewa kwa hiyo baada ya
siku tano hadi saba watakufa.
Mifuko ya tabaka tatu ya PICS imetengenezwa mahsusi kwa
teknolojia ya “hermetic” yaani isiyopitisha hewa, hivyo kuwanyima hewa ya
oxygen wadudu ambao ni viumbe hai wanaohitaji hewa kuendelea kuishi. Mifuko
miwili ya ndani isiyoingiza hewa na mmoja wan je wenye alama ya PICS – Purdue
Improved crops storage.
Mifuko ya PICS imezinduliwa rasmi katika ukumbi wa bunge
mnamo tarehe 13 June 2016 na Naibu spika wa bunge la Jamhuri wa muungano
Mheshimiwa Dokta Ntulia Hudson na kuhudhuriwa na wabunge na mawaziri akiwemo
waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mheshimiwa Charles Mwijage na Naibu
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Ole Nasha.
Mmoja wa wakulima mwenye ushahidi wa kutumia mifuko ya
PICS, Akbarual Mshana ameeleza kuwa “mwezi wa nane 2014 nilihifadhi mahindi
yangu bila kuyawekea dawa huku yakiwa na wadudu ndani kwenye mfuko mmoja wa
PICS ili niweze kuthibitisha kama kweli hayatameng’enywa na nikaufungua mfuko
mwezi wa tatu 2016, mahindi yalikuwa safi kabisa hata wale wadudu wote walikuwa
wamekufa, hapo ndipo nikaamini kweli mifuko ya tabaka tatu ya PICS inasaidia
kulinda mazao yangu”
Mifuko ya PICS inatokana na kuwepo kwa wadudu waharibifu
wanaoshambulia mazao ghalani na hasa dumuzi ambao huharibu mazao ya wakulima
masikini katika nchi zinazoendelea. Teknolojia hii ilibuniwa katika miaka ya
1980 na Idara ya elimu ya wadudu (Entomology) ya Chuo Kikuu cha Purdue, kwa
kushirikisha na wanafunzi, wafanyakazi na wadau kutoka Cameroon Kaskazini kwa
msaada wa USAID.
Mradi wa Mifuko ya PICs ililetwa nchini Tanzania mwezi
Julai mwaka 2014 na Chuo Kikuu cha Purdue – Indiana, Marekani kwa kushirikiana
na kiwanda cha PPTL kilichopo Tanga, ambacho kina uwezo wa kuzalisha mifuko
2,400,000 kwa mwaka. Toka Julai mwaka 2014 hadi Mei 2016 mifuko 470,000
imeshatengenezwa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Mifuko ya PICS ni teknolojia yenye ubora, rahisi kutumia
katika ngazi ya kaya na pia hupunguza matumizi ya kemikali hivyo kuhakikisha
usalama wa chakula. Huko Afrika Magharibi, teknolojia hii imeweza kutumika kwa
takriban miaka tisa na baada ya mafanikio makubwa katika nchi hizo za Afrika
Magharibi mradi huu umesambazwa katika nchi saba ambazo ni Malawi, Uganda,
Ethiopia, Nigeria, Ghana, Burkina Faso na Tanzania.
Mifuko hii imetengenezwa kwa ujazo wa kilogram 100 na
inatumika kuhifadhi nafaka za aina zote kama vile mahindi, mtama, uwele, ulezi,
ngano pamoja na mazao yote ya jamii ya mikunde.
No comments:
Post a Comment