Aliugua kiharusi wiki mbili
zilizopita na hali yake ikawa mbaya zaidi ghafla Jumanne.
Bw Peres, ambaye alikuwa mmoja wa
waliosalia kutoka kwenye kizazi cha wanasiasa waliokuwepo wakati wa kuundwa kwa
taifa la Israel mwaka 1948, alihudumu kama waziri mkuu wa nchi hiyo mara mbili
na mara moja kama rais.
Alishinda tuzo ya amani ya Nobel
mwaka 1994 kwa mchango wake katika mashauriano yaliyopelekea kutiwa saini kwa
mkataba wa amani kati ya Israel na Palestina mwaka mmoja awali.
Wakati mmoja, aliwahi kusema kwamba
Wapalestina ndio "majirani wa karibu zaidi" wa Waisraeli na wanaweza
kuwa "marafiki wa karibu zaidi".
Bw Peres amefariki akitibiwa katika
hospitali moja iliyopo karibu na mji wa Tel Aviv mapema Jumatano, jamaa zake wa
karibu wakiwa karibu naye.
Alikuwa amelazwa chumba cha
wagonjwa mahututi katika hospitali ya Sheba Medical Centre baada ya kupatwa na
kiharusi 13 Septemba.
Rais wa Marekani Barack Obama
amemweleza Bw Peres kama "rafiki wa karibu" kwenye taarifa, na
akasema: "Aliongozwa na maono ya heshima na utu na alifahamu kwamba watu
wenye nia njema wanaweza kustawi pamoja."
Bw Peres alitunukiwa Tuzo ya Amani
ya Nobel kwa pamoja na Waziri Mkuu Yitzhak Rabin, ambaye baadaye aliuawa, na
Kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat.
Shimon Peres alikuwa nani?
§
Alizaliwa 1923 Wisniew, Poland, eneo ambalo sasa hufahamika kama
Vishneva, Belarus
§
Alichaguliwa kwenye Knesset (Bunge la Israel) mara ya kwanza
mwaka 1959
§
Alihudumu katika serikali 12, mara moja kama rais na mara mbili
kama waziri mkuu.
§
Alitazamwa kama mpenda vita miaka yake ya awali - aliongoza
mashauriano ya kuitafutia silaha Israel ilipokuwa bado taifa changa
§
Alikuwa kwenye serikali iliyoidhinisha sera ya kujengwa kwa
makazi ya Wayahudi katika maeneo ya Wapalestina yaliyotekwa na Israel
§
Hata hivyo, alitekeleza mchango muhimu katika kupatikana kwa
Mkataba wa Amani wa Oslo, mkataba wa kwanza kati ya Israel na Wapalestina,
uliosema wangefanya juhudi "kuishi kwa amani pamoja".
Mwanzoni mwa maisha yake kisiasa, alipewa jukumu la kusimamia
wanajeshi na ununuzi wa silaha za kutumiwa na Haganah, jeshi la Israel.
Aliingia kwenye mkataba na Ufaransa wa kuipa Israel ndege za
kivita aina ya Mirage. Aidha, alisaidia kuanzisha kiwanda cha siri cha nyuklia
cha Israel.
Alikuwa waziri wa ulinzi mwaka 1976, watekaji nyara kutoka
Palestina walipoteka ndege ya Israel na kuielekeza hadi Entebbe, Uganda.
Aliongoza juhudi za kuwaokoa zaidi ya mateka 100.
Zamani alitetea makao ya walowezi wa Kiyahudi Ukindo wa
Magharibi lakini baadaye akageuka mtetezi mkuu wa amani. Mara nyingi,
alizungumzia haja ya kutokuwa na msimamo mgumu kuhusu maeneo ya ardhi ya
Wapalestina.
Aliendelea kutekeleza shughuli nyingi za umma uzeeni, kupitia
shirika lake lisilo la kiserikali la Peres Centre for Peace, ambalo hutetea
uhusiano wa karibu baina ya Waisrael na Wapalestina.
Mwaka 2013 alisema: "Hakuna mbadala wa amani. Hakuna maana
ya kwenda vitani."
Alistaafu kutoka wadhifa wake kama rais mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment