Vitendo vya ukatilitili wa kijinsia
kwa watoto vimeendelea kuongezeka kwa kasi nchini katika kipindi cha mwezi
Januari hadi Julai mwaka huu ambapo zaidi ya watoto 2,570 wa kike na kiume
wamelawitiwa na kubakwa.
Akizungumza katika sherehe za
maadhimisho ya miaka 21 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
yaliyofanyika jana katika Makao makuu ya watoto yaliyopo Kurasini jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Helen Kijo-Bisimba alisema idadi hiyo ni
kubwa ukilinganisha na ya mwaka jana.
Hata hivyo, Mama Bisimba alisema
kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, takwimu hizo zinaweza kuwa ndogo
kutokana na kesi nyingi za ubakaji na ulawiti kwa watoto kutoripotiwa polisi
kwa sababu ya mila na desturi za maeneo mengi nchini.
“Ripoti ya Jeshi la Polisi kupitia
dawati la jinsia kati ya Januari na Machi 2016 inaonyesha matukio ya watoto
kubakwa na kulawitiwa yakiendelea kuongezeka kutoka 180 hadi 1765 hayo ni
matukio yaliyotolewa taarifa katika vituo mbalimbali vya polisi nchi nzima
ukilinganisha na matukio 1585 mwaka 2015. Hata hivyo waliohusika na matukio
hayo wameonekana wakirandaranda bila kuchukuliwa hatua za kisheria, ”alisema.
Alisema ripoti hiyo inaonyesha kuwa
kesi 1,203 zipo katika hatua ya upelelezi, 822 zipo mahakamani na watuhumiwa
234 wamekwisha hukumiwa.
“Pia utafiti uliofanywa na Shirika
la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto kwa kushirikiana na Tanzania kitengo
cha ustawi wa jamii unaonyesha kati ya watoto 10 wa kike 4 wamebakwa, na kati
ya watoto 10 wa kiume 3 wamelawitiwa zaidi ya mara tatu. Utafiti huo unaonyesha
kwa ujumla kuwa watoto wa kike na wa kiume 6 walifanyiwa ukatili huo na watu
ndani ya familia,” alisema.
Bisimba alisema asilimia 49 ya ukatili
hufanyika nyumbani, 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda shule au kurudi, na
asilimia 15 hufanyika shuleni. Pia ripoti hiyo ya UNICEF inaonyeaha kuwepo kwa
matukio ya watoto kulawitiana na kubakana wenyewe kwa wenyewe kutokana na
kuvizoea vitendo hivyo.
LHRC imeitaka serikali kupitia
Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya
Katiba na Sheria kuifanyia marekebisho sheria ya mtoto na kutilia mkazo malezi
bora kwa watoto ikiwemo kuweka kipengele kitakachotoa adhabu kali kwa familia
itakayoshindwa kutoa malezi bora kwa mtoto.
LHRC inayoshughulika na utetezi wa
sheria na haki za binadamu ilianzishwa Septemba 26, 1995.
No comments:
Post a Comment