Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo, jana alikuwa katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi
wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto mjini Arusha.
Tukio hilo lilitokea wakati
kiongozi huyo alipozungumzia mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo na kudaiwa
kupotosha ukweli wa mradi huo.
Katika maelezo yake, Gambo alisema
eneo la hospitali hiyo lilitolewa na familia ya Nyaga Mawalla, jambo
ambalo wananchi walilipinga wakishirikiana na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema (Chadema).
Hospitali hiyo itakayogharimu Sh
bilioni tisa, inajengwa kwa wafadhili ambao ni Taasisi ya Maternity Afrika,
Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na Mbunge Lema.
Kabla mkuu huyo wa mkoa hajazomewa,
alipewa nafasi ya kuzungumza na ndipo alipoeleza jinsi familia ya Mawalla
ilivyotoa eneo hilo.
Wakati akitoa kauli hiyo, Lema
ambaye alikuwapo mahali hapo, alisimama na kupaza sauti akisema, “mkuu wa mkoa
anapotosha ukweli wa mradi huu”.
Hatua hiyo ya Lema kulalamika
kwa sauti, iliwafanya wananchi nao kumzoea Gambo huku baadhi yao
wakimtuhumu kuingiza siasa katika shughuli za maendeleo.
Kutokana na zomeazomea hiyo,
polisi waliokuwapo mahali hapo wakiwa na silaha za moto na mabomu ya
machozi, walilazimika kusogea eneo la meza kuu huku wengine wakimzunguka Gambo
aliyekuwa akiendelea kubishana na Lema kuhusu ukweli wa mradi wa hospitali
hiyo.
“Huyoo, acha kupotosha ukweli
wewee, usilete siasa kwenye maendeleo, huyooooo,” zilisikika sauti za wananchi
kutoka upande wa pili wa meza kuu huku Lema naye akisikika akihoji kwa nini
mkuu huyo wa mkoa alikuwa akisema uongo.
Katika hotuba yake ambayo pia
ilikatishwa baada ya kutokea kelele hizo, Gambo aliishukuru familia ya marehemu
Mawalla kwa kile alichosema ilitoa eneo hilo na kuwatafuta wafadhili wa kujenga
hospitali hiyo.
“Hili wazo lilikuwa ni la familia
ya Mawalla kwa sababu ardhi ni mali yao na walikuwa na maono ya kujenga
hospitali hii.
“Kwa hiyo, Serikali itakuwa pamoja
nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnafanikiwa,” alisema Gambo huku akizomewa na
wananchi.
Wafadhili kutoka Ulaya waliokuwa
kwenye uzinduzi huo, walijikusanya makundi na kumkumbatia Mtendaji Mkuu wa
Taasisi ya Maternity Afrika, Andrew Brown, wakimpa pole kwa kile kilichotokea.
Hata hivyo, baadhi ya wafadhili hao
walianza kulia wakionyesha ni kwa kiasi gani hawakuridhishwa na mvutano kati ya
mkuu wa mkoa, mbunge na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari
baada ya uzinduzi huo, Lema alisema mkuu huyo wa mkoa alifanya makosa
kuupotosha umma kuhusu mradi huo.
“Mkuu wa mkoa alitakiwa kufika saa
4.00 asubuhi lakini hakuonekana kwa madai kwamba asingeweza kuja kama mimi
nipo.
“Ilipofika saa saba kasoro bila
kumuona, nikampigia simu Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi kumweleza suala
hili, naye akampigia simu Katibu Mkuu Tamisemi.
“Inavyoonekana Tamisemi walimpigia
simu mkuu wa mkoa ndipo akaamua kuja akiwa amechelewa.
“Kwa hiyo, kilichofanyika hapa
kinaonyesha aina ya viongozi walioaminiwa na Rais John Magufuli wamsaidie
kuongoza nchi.
“Wafadhili walimualika kuipa
heshima Serikali, lakini hakuonekana hadi alipopewa maagizo.
“Kwa faida ya wasiofahamu ni kwamba
mimi kupitia ArDF ndiyo tuliotafuta ardhi kwa marehemu Nyanga Mawalla.
“Kibaya zaidi, alipofika hapa
akaagiza ratiba ibadilishwe mimi nisizungumze kwa sababu anazozijua yeye.
“Ushahidi wa ratiba hiyo ni kwamba,
ilipangwa azungumze mtendaji mkuu wa Maternity Afrika, kisha mkurugenzi wa
ArDF, baadaye mimi mbunge pamoja na Mawalla kutoa historia ya mradi na mwisho
mkuu wa mkoa.
“Lakini, ratiba hiyo haikufuatwa na
badala yake alifanya anavyojua yeye mradi tu nisizungumze.
“Sasa, hivi unawezaje
kuwalazimisha Maternity Afrika wasinilete mimi wakati kwenye mkataba wa
hili eneo mimi na ArDF ndiyo wasimamizi wa mradi?” alihoji Lema.
Mwenyekiti wa ArDF, Elifuraha Mtoi,
alisema Taasisi ya ArDF kwa kushirikiana na Lema ndiyo waliofanikisha mradi
huo.
“Hizi ni jitihada binafsi za ArDF
kwa sababu baada ya kupata wafadhili, tuliwaunganisha na Mawalla Trust
ambao ndiyo wamiliki wa maeneo haya.
“Kwa hiyo, kilichofanywa na mkuu wa
mkoa kimetufedhehesha mbele ya wafadhili,” alisema Mtoi.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Maternity
Afrika (Brown), alisema fedha za ujenzi wa hospitali hiyo zitatokana na
michango mbalimbali ya wafadhili na sadaka kutoka makanisani.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Arusha, Amani Golugwa ambaye pia ni mmoja wa waaanzilishi wa Taasisi ya ArDF,
alimtangaza Gambo kama adui wa maendeleo mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment