Mtoto Isack Ernest (16)
anayetuhumiwa kuwa ni mhalifu, maarufu Panya Road, amezinduka akiwa chumba cha
kuhifadhia maiti (mochwari) katika Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.
Isack ni miongoni mwa vijana watano
waliopigwa na wananchi wenye hasira kwa madai ya kuiba mali zao hali
iliyosabisha apoteze fahamu na kudhaniwa amefariki dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi, Gilles Muroto, alisema baada ya polisi kupigiwa simu na
raia wema kuwa kuna vijana watatu wamefariki dunia, walikwenda eneo la tukio na
kuwakuta wakiwa na hali mbaya.
“Mmoja wao anayeitwa Kelvin
Nyambocha (14) alifariki dunia baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi.
“Kabla ya kufariki, Kelvin
alifuatana na wenzake kwa lengo la kwenda kuangalia tamasha la kuibua vipaji
vya muziki wa singeli lililoandaliwa na Radio Clouds Fm lililofanyika Mbagala
Zakhem,” alisema Kamishna Muroto.
Alisema wakati wanarudi nyumbani,
kundi la vijana hao wanaojiita Panya Road waliokuwa na silaha za jadi
(mapanga), waliwavamia watembea kwa miguu na kuwaibia mali zao na ndipo
wananchi walipofanikiwa kuwakamata watano.
Alisema Isack alipigwa hadi
akazimia kiasi ambacho walijua amefariki dunia na ndipo alipopelekwa chumba cha
kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo na
kuwekewa namba tayari kwa kuingizwa kwenye jokofu.
“Wakati amewekwa chini kwa ajili ya
kuingizwa kwenye jokofu, alizinduka kwa kupumua na kuonekana bado yupo hai,
hali iliyosababisha kupelekwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU),”alisema Kamishna
Muroto.
Alisema baada ya kupata fahamu na
afya yake kutengemaa, alihojiwa na Jeshi la Polisi, akawataja wenzake 10
waliokuwa kikundi kimoja. Vijana hao ni Menso Somba (16), Adam Jumanne (16),
Bakari Amir (14), Ally Said (17), Abdillah Yusuf (16), Brown Mathias (15),
Jafari Salum (13), Hamisi Mwanda (16), Siraji Hamisi (16) na Jeremia Gaudence
(13).
Wakati vijana hao wakipewa mapanga
yao mbele ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Temeke huku wazazi wao wakishuhudia,
walianza kuyagombea wengine wakidai kuwa yao yamebadilishwa na kupewa wenzao.
Kamishna Muroto alisema kikundi
hicho kina bendera inayoonyesha michoro mbalimbali ikiwamo askari mwenye silaha
anakimbia huku anatiririka damu, mtu ameanguka chini akiwa amekatwa mkono,
nyumba na vijana wawili wakiwa wameshika panga.
Alisema kundi hilo la vijana ambalo
linazunguka maeneo mbalimbali, limekuwa likijiita ‘Taifa Jipya’.
Kamishna Muroto alisema kijana
mwingine, Faraji Suleiman (19) ambaye pia hali yake ni mbaya, amelazwa Hopitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kamanda Muroto alisema vijana
wawili aliowataja kuwa Hamisi Mponda (18) na Abdallah Omari (15) walitibiwa
hospitali ya Temeke na kuruhusiwa.
Alisema jeshi hilo kupitia Sheria
ya Watoto ya mwaka 2009 kifungu 7-9, linakusudia kuwafikisha mahakamani wazazi wa
watoto 16 ambao walitajwa na kuthibitisha kufanya uhalifu huo, kwa kushindwa
kuwaangalia watoto wao.
Kamishna Muroto alisema wazazi wana
wajibu wa kuhakikisha mtoto anakuwa chini ya uangalizi ambao hauwezi
kumsababishia madhara ya kimwili na kisaikolojia.
“Hii ina maana kila mzazi
ahakikishe mtoto wake ana ulinzi, yuko salama muda wote dhidi ya udhalilishaji
na hatari zote ili watoto hawa wakue vizuri,” alisema Kamishna
Muroto.
Alisema jukumu la mzazi ni
kuhakikisha mtoto anakuwa kwenye malezi bora na si kumwacha akilelewa na
walimwengu.
“Mzazi atakayeshindwa kumsimamia
vyema mtoto wake na kukiuka sheria ya mtoto ya mwaka 2009 katika kifungu cha
14, atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atafungwa miezi 6 au kulipa faini
ya Sh milioni 5,” alisema Kamanda Muroto.
Alisema kutokana na mazingira
waliyokutwa watoto hao, wazazi wao wanatuhumiwa kwa kukiuka sheria hiyo ya
watoto.
Akisimulia mkasa huo, Isack Ernest
alisema yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na
hajawahi kufanya vitendo vya kihalifu.
Alisema wakati yupo kwao, wenzake
walimfuata na kumwambia waende kwenye tamasha la singeli Mbagala.
“Tulienda na baada ya kumaliza
tamasha, wenzangu wakasema twende tukale (walimaanisha wakapore), mimi nikajibu
sina pesa, ndipo waliposema wakienda kula hawatanigawia kwa kuwa aliyekula
kala, ndipo walipokwenda kuvamia watembea kwa miguu na kuiba.
“Wakati nikiwa ng’ambo ya pili,
nikasikia sauti ya watu wanasema mwizi mwizi, mwizi,” alisema
Isack.
Alisema baada ya kupigiwa kelele za
wezi, walikimbia na kumfuata alipo ndipo kipigo kilipomwangukia yeye hadi
kupoteza fahamu.
“Nilikuja kushtuka nipo ICU, huku
nikiwa sijui niko wapi, nimekoma kujihusisha na makundi kwa sababu sijawahi
kuiba katika maisha yangu,” alisema Isack.
Baba mzazi wa kijana huyo, Ernest
Chalo, alisema mtoto wake alimuaga anakwenda kuangalia mpira Mbagala Oktoba 15,
mwaka huu.
Alisema wakati yeye anafuatilia
mchezo wa timu ya Simba na Kagera Sugar, alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu
akimpa taarifa ya kuwa mtoto wake amefariki dunia.
“Kiukweli nilichanganyikiwa kwa
sababu nimetoka kumzika mke wangu wiki moja iliyopita, tena napokea taarifa ya
mtoto kufariki, nilitoka mpaka kwa mwenyekiti wangu wa mtaa na kumpa taarifa,
nikachukua usafiri wa pikipiki kwenda Hospitali ya Temeke,” alisema
Chalo.
Alisema alipofika hospitalini hapo,
aliambiwa mtoto wake yupo chumba cha kuhifadhia maiti, lakini alipoletewa mwili
kuutambua haukuwa wa mtoto wake, ndipo akatokea msamaria mwema akamwambia mtoto
wake alizinduka.
“Kutokana na baridi kali ya chumba
cha kuhifadhia maiti, mtoto wangu alipoingizwa mle ndani alipumua na hivyo
kuhamishiwa ICU,” alisema Chalo.
No comments:
Post a Comment