Watu sita wanaotuhumiwa kuwa
majambazi hatari, wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika eneo la
Mbezi kwa Yusuf Makondeni katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa
Kanda Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, watuhumiwa hao waliuawa
katika majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa
Kutumia Silaha.
Mkondya alisema wamepata taarifa
kutoka kwa raia mwema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha, wamejipanga
kufanya tukio la ujambazi kwa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa
akitoka Benki ya Diamond Trust Bank (DTB), tawi la Barabara ya Nyerere, ambaye
angepita katika barabara hiyo kwenda mkoani Morogoro.
Alisema baada ya kupata taarifa
hizo, polisi waliweka mtego na majambazi hao wakitumia gari aina ya Toyota
Carina lenye namba za usajili T970 DGZ rangi ya fedha, walionekana wakilifukuza
gari la mfanyabiashara huyo, kisha kulipita na kumsimamisha kwa nguvu.
“Majambazi wawili wakiwa na bastola
walishuka katika gari hilo. Baada ya kugundua kuwa wameingia kwenye mtego wa
polisi, walianza kufyatua risasi kwa askari wakitumia bastola na wenzao
waliokuwa wamejaa kwenye gari yao walianza kushuka huku wakifyatua risasi
kuelekea kwa askari,” alisema Kaimu Kamanda Mkondya.
Alisema kutokana na hali hiyo,
askari walianza kujibu mashambulizi na kuwaua majambazi hao na baada ya
upekuzi, zilipatikana bastola mbili, moja ya kijeshi aina ya Chinese ikiwa na
risasi moja ndani ya kasha la risasi; na nyingine aina ya Browning ikiwa
imefutwa namba zake na maganda sita ya risasi yaliyookotwa katika eneo la
tukio.
Miili ya watuhumiwa hao
imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na upelelezi unaendelea
ili kubaini mtandao mzima wa ujambazi.
Katika tukio lingine la Oktoba 17,
mwaka huu saa 2:00 usiku katika maeneo ya Tegeta Masaiti, watuhumiwa watatu wa
ujambazi wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki aina ya Fekon yenye namba MC370
BEY, wakiwa na bunduki aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na kitako, walivamia
duka la Abdallah Juma (46), mkazi wa Tegeta na kupora fedha za mauzo na kuiba
vocha za mitandao mbalimbali, ambazo thamani yake haijafahamika.
“Polisi baada ya kupata taarifa
waliwafukuza majambazi hao, walipoona wanakaribiwa na askari, walitupa chini
begi walilokuwa nalo na kutelekeza pikipiki yao kisha kukimbia, begi
lilipopekuliwa lilipatikana na silaha hiyo,” alisema.
Aidha, wananchi wenye hasira
waliendelea kuwakimbiza majambazi hao na kumuua mmoja huku wengine wakikimbilia
kusikojulikana.
Katika hatua nyingine, Mkondya alisema wamekamata watuhumiwa wawili wa unyang’anyi kwa kutumia nguvu wakiwa na pikipiki moja na funguo bandia 75.
Katika hatua nyingine, Mkondya alisema wamekamata watuhumiwa wawili wa unyang’anyi kwa kutumia nguvu wakiwa na pikipiki moja na funguo bandia 75.
Alisema watuhumiwa hao, Ally
Makwega (53) mkazi wa Tandika na Fabian Greyson (39) mkazi wa Yombo walikamatwa
Oktoba 4, mwaka huu saa 6:00 usiku.
Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa
na pikipiki yenye namba MC292 AMD aina ya Boxer rangi nyekundu, wanayoitumia kufanya
uhalifu, wakiwa na funguo bandia 75 ambazo huzitumia katika kuvunja nyumba
mbalimbali ya biashara za kulala wageni, maghala ya kuhifadhia bidhaa na
maduka.
Baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa,
walikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya uvunjaji wa maghala na kuiba katika
mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Watuhumiwa hao watafikishwa
mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment