WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam
Alexander (pichani mwenye mafaili) kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja
na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya
Lindi.
Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi
huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Bw. Stephen Chami na kumuelekeza
afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana
Jumatano, Oktoba 19, 2016 wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ng'apa
ambapo aliagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo,
Mhandisi Idrisa Sengulo.
"Kamanda wa TAKUKURU fanya
mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa Wizarani, mimi najua
analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar es Salaam kama inalingana
na siku alizokaa,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Mhandisi hiyo anakabiliwa na tuhuma
mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara
bila la kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha
posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu alisema Serikali
haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa
dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi. "Huyu
nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam."
Alipoulizwa sababu za kutokuwepo
ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa Dar es
Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatulia changamoto mbalimbali
zinazoikabili mamlaka hiyo.
"Unatumia siku ngapi kuandika
proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na unakaa Dar es Salaam
hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu! Tena badala ya kulipwa
sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa sh.150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,”
amesema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake
siku tatu mkoani Lindi na amerejea jijini Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU
No comments:
Post a Comment