Kamati ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala imekataa mapendekezo ya kufanyia marekebisho Sheria ya Leseni
za Uchukuzi ya mwaka 1973 yenye lengo la kuongeza kiwango cha adhabu ya faini
hadi kufikia asilimia 500 kwa watakaokiuka masharti ya leseni hizo.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa
mbele ya kamati hiyo mjini Dodoma jana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi
Kavu (Sumatra).
Baada ya kuyakataa mapendekezo
hayo, kamati hiyo imetoa muda wa siku mbili kwa Sumatra kuhakikisha
inawasilisha mbele ya kamati hiyo mapendekezo yanayokubalika.
Sumatra inapendekeza kuongeza
kiwango cha adhabu ya faini kutoka kati ya Sh 10,000 na Sh 50,000 hadi Sh
200,000 na 500,000 kwa watoa huduma za uchukuzi, watakaokiuka masharti ya
leseni zao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed
Mchengerwa alisema mapendekezo hayo, yatazidi kuwaongezea mzigo Watanzania
badala ya kuwasaidia.
Alisema kiwango hicho cha faini
kubwa, kamwe hakitazuia tatizo la ajali za barabarani, zaidi ya kuongeza ukubwa
wa tatizo la rushwa.
“Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga kuwasaidia wananchi, lakini mapendekezo haya yatazidi kuwaongezea
mzigo kwa sababu kiwango cha faini hizi kama kitapitishwa, watoa huduma za
uchukuzi watahamishia hasara yao kwa wananchi,” alisisitiza.
Aliitaka mamlaka hiyo, kwenda
kuyafanyia kazi tena mapendekezo hayo kwa kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na kuwasilisha viwango vya faini vinavyokubalika.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo,
Joseph Mhagama ambaye pia ni mbunge wa Madaba, alisema mapendekezo hayo hayana
nyongeza yoyote, itakayoisaidia serikali katika kudhibiti tatizo la ajali
barabarani.
“Kwa sasa serikali imeweka nguvu
zake katika kupunguza ajali za barabarani, lakini kiwango cha faini hizi hakina
uhusiano wowote na jitihada hizi zaidi ya kuiongezea Sumatra mapato na kuwapa
mzigo walipa kodi,” alisema.
Akiwasilisha mapendekezo ya mamlaka
hiyo mbele ya Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema
mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, yamelenga kuiboresha zaidi
sheria hiyo ya leseni za uchukuzi.
Alisema marekebisho hayo, pia
yatasaidia mamlaka hizo kuendana na mahitaji ya sasa hasa katika eneo la adhabu
ya faini, hali itakayopunguza kiwango kikubwa cha kukiukwa kwa masharti ya
leseni hizo za uchukuzi.
No comments:
Post a Comment