Wakati leo ni mwaka mmoja tangu
matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar yafutwe Oktoba 28, 2015, Katibu Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad amemtuhumu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC), Jecha Salim Jecha kuwa ndiye aliikwamisha nchi kwa kupindua maamuzi ya
wananchi.
Maalim Seif alisema kutokana na uamuzi huo, ndiyo maana mpaka
sasa mwenyekiti huyo ameshindwa kuibuka hadharani akielewa alibeba dhima ya
Wazanzibari na Watanzania wote wapenda amani.
Maalim Seif aliyasema hayo jana
alipofanya ziara ya siku moja katika wilaya zote saba za Unguja katika
kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Jecha alipofuta uchaguzi huo.
Maalim Seif aliita siku hii ‘black
October’ akisema ndiyo siku Jecha alitekeleza kwa makusudi kufuta ndoto ya
Wazanzibari ya kupata viongozi wanaowataka.
“Jecha ndiye aliyesitisha ndoto
yetu ya kuwa Singapore, alipindua demokrasia na kufuta matokeo bila ya kuwapo
kifungu chochote cha Katiba kinachotoa mamlaka hiyo,” alisema Maalim
Seif.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais
mstaafu, alisema kuwa kabla ya Jecha hajatekeleza azma hiyo ovu, waangalizi
wote wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi na ZEC wenyewe walijiridhisha na
kutoa tamko kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Waangalizi hao ni pamoja na Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Bara la Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU).
“Nasema alichotekeleza Jecha ni
dhuluma na mapinduzi ambayo yalilenga kupindua maamuzi halali ya wananchi wa
Zanzibar,” alisisitiza Maalim Seif akiwahutubia viongozi na watendaji wa
CUF wa wilaya za Unguja.
Alisema yeye na viongozi wenzake
wamekuwa wakiwatuliza wananchi na kwenda nao bega kwa bega, wakielewa hakuna
popote umma ulipodai haki yao duniani kwa njia za kistaarabu na za kidemokrasia
wakashindwa.
“Hivyo tambueni kuwa kimya kingi
kina mshindo na haki yetu iliyoporwa haipo mbali kuipata kwani baada ya dhiki
ni faraja,” alisema Maalim Seif.
“Jueni kuwa katika kutekeleza hayo
zipo njama za waziwazi za kutaka kuipitisha Katiba ambayo haikupendekezwa na
Watanzania kupitia maoni yaliwasilishwa kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba,” alisema Maalim
Seif.
Maalim Seif alisema miongoni mwa
njama hizo ni mazungumzo yanayoendelea sasa kujaribu kuibua utaratibu wa kura
ya maoni ili kuipitisha Katiba hiyo, chini ya usimamizi wa ZEC na NEC.
Alisema miongoni mwa njama za
kuififisha Zanzibar ni mpango wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi na
kuwakosesha wananchi fursa ya kufaidi raslimali zao.
Jecha hakupatikana jana kuzungunzia
madai hayo, lakini Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipoulizwa
alisema kwa sasa wapo katika mkakati wa kuimarisha chama katika ngazi zote
yakiwamo matawi yao.
“Unajua sisi hatuzungumzii tena
hayo, uchaguzi ulikwishafanyika na Serikali ikaundwa na sasa inafanya kazi, la
msingi tunaimarisha chetu,”alisema Vuai aliyeko katika ziara ya kichama kisiwani
Pemba.
Akizungumza katika ofisi za CUF
Wilaya ya Kati Unguja, Maalim Seif alisema, “Nataka nikwambieni
kilichotendeka kupitia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar hivi karibuni wakidai
kujadili sheria ya uchimbaji mafuta, ni kiini macho tu, maana hatujaona mabadiliko
yoyote katika Katiba ya Jamhuri tukielewa kwamba jambo hilo bado ni suala la
Muungano.”
Maalim Seif alihoji pia uhalali wa
tamko la SMZ wa kumzuia asiongee na wananchi misikitini, akisema hiyo ni katika
njama za kumnyamazisha asiyaeleze hayo.
Hivi karibuni, Waziri wa Nchi,
Ofisi za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed alipiga
marufuku hatua ya Maalim Seif kutembelea na kuongea na wananchi misikitini.
Kufuatia hatua hiyo Maalim Seif
alihoji akisema, “Je, Mohamed Aboud haelewi wajibu wake, mbona
hatujamsikia akikemea uvunjwaji wa Katiba na pia ukiukwaji wa Sheria Na. 5 ya
Vyama Vingi vya Siasa ya Mwaka 1992, inayotoa ruhusa kufanya mikutano na
maandamano, hayaoni hayo, hajui kuwa yamepigwa marufuku kinyume na Katiba?”
No comments:
Post a Comment