Shirika la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) limekiri kuwapo ubadhirifu kwenye mkataba wa ubia na Kampuni ya
Azimio Housing Estates iliyotakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi Kigamboni
na kuna hatari ya kupoteza Sh bilioni 270.
NSSF pia imekiri ubadhirifu katika
utoaji mikopo kwenye Saccos mbalimbali nchini ikiwamo ya Bumbuli, inayoonekana
kukopeshwa zaidi ya Sh bilioni mbili, bila kuwa na sifa huku kukiwa pia hakuna
kumbukumbu ya mwaka mzima kama walirudisha mkopo wa awali.
Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa
Samuel Wangwe alieleza jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) kwamba Bodi yake ilipoingia madarakani iligundua ubovu wa mkataba huo na
kusitisha kutoa fedha na sasa inaangalia namna ya kujitoa bila kupoteza fedha
zilizowekezwa.
Alisema uwekezaji huo ambao ardhi
ya mwekezaji ilipaswa kuwa ekari 20,000, hatua ya awali ulipaswa kuanza na
ekari 300, lakini uchunguzi uliofanyika hivi karibuni ulionesha kuwa kuna ekari
3,500 pekee hali inayoonesha udanganyifu uliofanyika tangu awali.
Pia mwekezaji huyo alidanganya
uhalisia wa bei ya ardhi hiyo, kwani alionesha kuwa thamani ya ekari ya moja ni
Sh milioni 800 wakati kiuhalisia, ardhi hiyo thamani yake ni Sh milioni 25 peke
yake.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa
Kaboyoka alisema imekuwa vigumu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuthibitisha uwepo wa viwanja hivyo kwa kukosekana
hatimiliki, umiliki wa ekari 19,700 za ardhi ambazo ni sehemu ya mtaji wa
Azimio Housing Estates kwa asilimia 20, hivyo fedha za NSSF zinakuwa kwenye
hatari ya kupotea.
Alisema NSSF ambayo inamiliki hisa
ndogo kuliko Azimio, imewekeza fedha nyingi, zaidi ya dola milioni 129 za
Marekani wakati mbia huyo aliwekeza dola milioni 5.5.
Akijibu hoja za Mwenyekiti huyo,
Profesa Wangwe alisema mradi huo ulisimama tangu Februari kutokana
na mbia kukosa fedha na kwamba hakopesheki kwani NSSF inamdai.
Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige
alisema mradi huo wa Kigamboni ni mchafu na katika mazingira hayo ambayo Bodi
pia imeshituka kuwa mchafu hivyo ni vema NSSF ingejitoa kuliko
kuendelea na mkataba mbovu.
“Ni vema ukishagundua kuwa
unachezea kitenesi kichafu ambacho kilianza kuchezewa na watu ambao
wameshaondolewa, usiendelee kucheza na mtu yule yule ili asije kukuingiza
katika matatizo makubwa zaidi,” alisema Maige.
Profesa Wangwe alisema ni vigumu
kujitoa haraka kwenye mkataba huo, kutokana na fedha nyingi waliyowekeza ambayo
iko hatarini kupotea na kwamba ardhi yote ni ya mwekezaji huyo hivyo wanatafuta
namna ya kurudisha fedha waliyowekeza hata kama haitakuwa na faida.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh
Hilaly alihoji kama mkataba unaruhusu mwekezaji huyo kukopa ili kuendeleza
mradi huo.
Mkurugenzi wa NSSF, Profesa Godius
Kahyarara alisema mwekezaji huyo alitaka kukopa NSSF ili aendeleze mradi huo
ambao umesimama lakini hakopesheki kwa kuwa anadaiwa.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge
walihoji uhalali wa Saccos kukopeshwa mara mbili kwa mwaka, huku zingine
zikikosa mikopo na vigezo vilivyotukia katika kutoa mikopo hiyo.
Kuhusu Saccos ya Bumbuli, Kaboyoka
alisema mbunge wake anafahamika, hivyo inashangaza ipewe fedha hizo kwa mwaka
mmoja na kuhoji sifa zilizotumika kuzitoa wakati Saccoss zingine hazijapata.
Alisema ni vema ufanyike ukaguzi
maalumu kwenye Saccos hiyo kwani fedha hizo ni mafao ya wafanyakazi ingawa pia
inatia shaka katika utoaji, kwani awali Saccos hiyo ilipewa zaidi ya Sh bilioni
moja na kwamba hesabu hazioneshi, kwamba fedha hizo zilirejeshwa, lakini ndani
ya mwaka mmoja ikapewa fedha zingine.
NSSF ilitoa mikopo kwa Saccos tisa
kwa kiasi kinachozidi asilimia 50 ya thamani ya mali za Saccos husika, kinyume
na sera ya Shirika ya kukopesha na ziliomba kiasi ambacho hazikustahili.
Katika ripoti ya CAG mbali na
Bumbuli, Saccos zingine zilizopewa fedha nyingi ni Korongo Amcos, UMMA, SBC,
Hekima, Ukombozi, Uzinza, Harbour na Umoja.
Akijibu hoja hizo, Profesa Wangwe
alisema Saccos zilizopewa fedha zaidi ya mara mbili kwa mwaka ikiwamo ya
Bumbuli iliyopewa Sh bilioni 2.473 kwa mwaka 2014/15, wakati anaingia kwenye
nafasi hiyo, aliliona hilo kama tatizo hivyo kuagiza kufanyike ukaguzi maalumu.
Alisema waliokuwa wanasimamia
Saccos hizo walisimamiswa kazi tangu Bodi mpya ilipoingia na kwamba walisitisha
kutoa mikopo ya aina yoyote katika Saccos zote nchini, hadi uongozi wa Shirika
utakapoanzisha utaratibu mpya.
“Watu wote waliohusika na
ubadhirifu wameshaondolewa ofisini, tulishituka kuona namna fedha hizo
zilivyotolewa, si zote zilizofika kwa wahusika, zingine ziliishia kwenye mikono
ya watu, tuliona ni vema ufanyike ukaguzi maalumu,” alisema Profesa Wangwe.
No comments:
Post a Comment