Kama mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema anapambana na Mrisho Gambo ili kujijenga kwa wananchi wake, basi
mkuu huyo wa mkoa ananufaika na vita hiyo na anatarajia makubwa zaidi baada ya
mzozo wa mwanzoni mwa wiki.
Wakati Gambo akitarajia kupandishwa
cheo na Rais John Magufuli, madiwani wa jiji hilo wametangaza kususia vikao
vyote hadi viongozi wa juu wa Serikali watakapoingilia kati mgogoro uliopo.
Wawili hao waliingia kwenye mzozo
mwingine mapema wiki hii wakati Gambo alipoalikwa kuzindua ujenzi wa hospitali
ya mama na mtoto, itakayojengwa kwa ufad kwa ufadhili wa taasisi ya Martenity
Africa alipojaribu kueleza historia ya kiwanja cha jengo hilo, maelezo ambayo
Lema aliyapinga kwa sauti kubwa na kusababisha shughuli hiyo kuvurugika.
Baada ya mzozo huo, Gambo amedokeza
kuwa kuna makubwa yanafuata.
“Baada ya hilo, simu zilikuja
kibao, lakini bahati nzuri kabla sijauliza kokote, na Mheshimiwa Rais ndio
akawa ananipigia akaniambia nina full confidence (nina imani) na wewe. Labda
wafikirie promotion (kupandisha cheo), lakini hayo mengine hayapo,” alisema
Gambo akiwaeleza wafanyabiashara wa mjini hapa kuhusu barua iliyosambaa juzi
kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais ametengua uteuzi wake.
“Baadaye (Rais) akaniambia kwamba
sasa ili (wafanyabiashara) wajue kwamba kweli nimekupigia simu, niitie mmoja
uliye naye karibu ili niongee naye. Ndio (mwenyekiti wa wafanyabiashara wa
Arusha) akapata previledge (bahati) naye ya kuongea na Mheshimiwa Rais.”
Iwapo Gambo atapandishwa cheo,
ambacho kwa mukhtadha wa utumishi wa umma chaweza kuwa ni kuteuliwa kuwa mbunge
na baadaye waziri, itakuwa ni mara ya pili kupanda cheo siku chache baada ya
kuzozana na Lema.
Gambo, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu
wa Wilaya ya Arusha Juni 26, alilumbana na Lema Agosti Mosi mbele na Naibu
Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo.
Katika tukio hilo, Lema alisema
Gambo haheshimu mipaka ya kazi zake, akimtuhumu kuingilia maamuzi ambayo tayari
yameshajadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri na kupitishwa na ofisi ya
mkuu wa mkoa katika kikao cha wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu
kata watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (Auwsa) jijini hapa.
“Nimeona nizungumze hapahapa ili
naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa mfano Baraza la Madiwani la mwaka
2008, ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi
120,000. Jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru
ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.
Hali hiyo ilimfanya naibu waziri
kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia changamoto hizo na kumpa nafasi
Gambo, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa wilaya, kujibu hoja hizo.
“Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi
ndiyo mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani. Muda wowote nina uwezo wa
kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa, hata kama yupo katibu tawala
na viongozi wengine,” alisema Gambo.
“Rais aliona ninafaa ndiyo maana
akaniteua na sihitaji kujifunza namna ya kuwa mkuu wa wilaya kwa kuwa huu
ni mwaka tano.”
Malumbano hayo yaliendelea na
kumuhusisha pia Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye aliungana na Lema
na madiwani wengine kupinga jambo hilo.
Baada ya vuta nikuvute hiyo mbele
ya waziri, Agosti 18 Gambo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua
nafasi ya Felix Ntibenda.
Siku chache baada ya uteuzi huo,
Gambo aliagiza halmashauri ya jiji kutafuta fedha za kupunguza deni la walimu
ambalo ni Sh154 milioni.
Mkurugenzi wa jiji hilo, Athuman
Kilamia alitangaza posho za madiwani ambazo zilikuwa zinalipwa kinyume cha
taratibu, zitumike kupunguza deni la walimu na zikatolewa.
Mgogoro ukaibuka kati ya madiwani
wa jiji hilo ambao wengi ni kutoka Chadema.
Sakata la Jumanne wiki hii linaweza
kumpa cheo kikubwa zaidi kutokana na Rais Magufuli kumpigia simu kwa lengo la
kumthibitishia kuwa yuko pamoja naye siku ambayo barua ya kughushi ilisambaa
kwenye mitandao ya kijamii kuwa mkuu huyo wa nchi ametengua uteuzi wa Gambo.
Sakata hilo lilitokea katika
uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto jijini Arusha
ambao utagharimu Sh9 bilioni, sehemu kubwa ya fedha hizo zikitoka taasisi ya
Martenity Africa.
Mvutano huo ulianza baada ya Gambo
kusema kuwa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali imetolewa na Taasisi ya
Mawalla Fund kwa kuwa muasisi wake, Nyaga Mawalla alikuwa na maono ya kusaidia
afya ya mama na mtoto.
Kauli yake ilikuwa ikimaanisha kuwa
Mfuko wa Maendeleo wa Arusha (ArDF) haikutoa kiwanja hicho kwa Martenity Africa
wala kutafuta mfadhili.
Jambo hilo liliwakera viongozi wa
ArDF, ambayo imeanzishwa na Lema na Elifuraha Mlowe, ambaye ni
mwenyekiti.
Lema alimtaka ndugu wa wakili huyo
amsahihishe Gambo, lakini hakuna kilichofanyika, ndipo aliposimama na kuanza
kupinga kwa sauti maelezo ya Gambo.
Lema alikuwa akisema mkuu huyo wa
mkoa anapotosha ukweli kwa misingi ya kisiasa, kwa kuwa Mawalla Fund ilitoa
kiwanja hicho kwa ArDF, ambayo ilitafuta wafadhili na kusaini nao mkataba wa
ujenzi wa hospitali.
Wageni kwenye hafla hiyo
iliyofanyika Bulka walijaribu kuwatuliza wawili hao, hawakufanikiwa kutokana na
Lema kuendelea kueleza kwa sauti kuwa Gambo anapotosha, huku mkuu huyo wa mkoa
akizungumza kwenye kipaza sauti kumtaka mbunge huyo atulie.
Shughuli hiyo ilimalizika kiutata
na hivyo waandaaji wakashindwa kuendesha harambee iliyopangwa kufanyika baada
ya uzinduzi.
No comments:
Post a Comment