Mchungaji Kiongozi wa Kanisa
la Assemblies of God (Mlima wa Moto), Getrude Rwakatare amesema ataendelea na
mpango wake wa kuwanusuru wafungwa wanaotumikia adhabu magerezani kwa kuwalipia
faini ili warejee uraiani.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana Dar es Salaam, alisema katika awamu ya pili ameamua kuwalipia wafungwa 43
waliopo katika magereza ya Mkoa wa Dodoma.
“Kampeni hii ya kuwalipia faini
kati ya Sh 50,000 hadi 200,000 wafungwa waliopo magerezani imetupa moyo na
Watanzania wengi wameguswa na hata kutupongeza. Kutokana na hali hii kanisa
letu sasa limefanya hivyo tena na safari hii tunaelekea mkoani Dodoma,” alisema.
Mchungaji Rwakatare alisema kesho
watawatoa wafungwa hao mkoani Dodoma ambapo vigezo walivyoangalia ni wanawake
wanaonyonyesha, wagonjwa na wazee.
“Nasi tunatimiza maandiko ya Mungu
katika kufanya hivi na kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Parole, Augustino
Mrema,” alisema Mchungaji Rwakatare.
Alisema kutokana na makosa
mbalimbali ya faini waliohukumiwa nayo wafungwa hayo, kanisa lao limetoa Sh
milioni 6.8 kwa ajili ya kulipia faini hizo.
Awali Rwakatare kupitia kanisa
lake, aliwalipia wafungwa 78 katika magereza matatu ya Keko, Segerea na Ukonga
ya jijini Dar es Salaam na kuachiwa huru baada ya kulipa faini ya Sh
milioni 25 zilizochangwa na waumini wa kanisa hilo.
No comments:
Post a Comment