Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema atahakikisha
anawachukulia hatua watendaji wote, walioshiriki katika udanganyifu wa kuingiza
kaya zisizostahili katika Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaosimamiwa na
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Aidha, aliiagiza Tasaf kuhakikisha
inafuatilia kaya zote ambazo ziliingizwa katika mpango huo bila kuwa na sifa
zinazostahili, kwa kuziorodhesha kwa majina, wanapoishi na kiasi cha fedha
walichopokea ili ripoti hiyo iwasilishwe kwa Rais John Magufuli.
Kairuki aliyasema hayo jana wakati
akizungumza baada ya kupokea ripoti ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Masikini (Tasaf III) ya Mkoa wa Dar es Salaam, sambamba na kuzungumza na
wananchi katika mitaa ya Kigogo Kati na Mikoroshoni, Manispaa ya Kinondoni.
“Kaya ambazo hazistahili hawafanyi
peke yao wanashirikiana na watu, kama ni viongozi katika ngazi za mitaa na kata
mitaa tunataka majina, na katika kila jina tujue nani alishiriki kumuingiza
nani alikuwa akimchukulia na kama yupo mtumishi wetu wa umma tujue ni nani na
hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa.”
“...Msije mkashangaa nikaja
kuelekeza polisi kukamata hawa na hawa kwa sababu hizi hela ni lazima zirudi,” alisema
Kairuki.
Alisema ameshapokea taarifa za
mikoa mbalimbali, lakini Dar es Salaam na wilaya zake bado na mwisho ilikuwa ni
Oktoba 6, mwaka huu, lakini aliwaongeza wiki moja ambayo tayari imeisha na
orodha hiyo inatakiwa ipelekwe kwa Rais Magufuli.
Kairuki aliongeza kuwa pamoja na
mkoa kusema umeondoa kaya 789 ambazo hazina sifa, lakini kuna kaya 5,457 ambazo
zinapaswa kuondolewa katika mpango huo kwa kuwa hazina sifa za kupokea ruzuku
hiyo.
“...baada ya kuelekeza uhakiki wa
nyumba kwa nyumba, sisi kwa taarifa tulizonazo tutaondoa kaya 5,457. Sasa
ujiulize nyinyi ndio mlikuwa katika zoezi na mkapata idadi hiyo, hapa inaonesha
kuna kitu hakipo sawa,” alisema.
Alisema katika kaya hizo
zitakazoondolewa, 1,867 hazina vigezo vya umasikini, 563 zipo kwenye orodha
lakini zilikuwa hazijitokezi kuchukua ruzuku na hazijulikani zilipo na kaya
nyingine 2,114 hazikupatikana wala kujulikana zilipo wakati wa ukaguzi.
Alisema kaya hizi ni nyingi na hasa
ikizingatiwa asilimia 76 hazijaingizwa katika mpango huo, hivyo kaya hizo
ambazo ziliandikishwa zinapaswa kwenda kukaguliwa ili ziweze kuingizwa katika
mpango huo ili katika awamu ya nane ya uhawilishaji fedha waweze kupata.
Kairuki alisema kiasi kikubwa cha
fedha kimepotea, ambacho kingeweza kuwasaidia watu wanaostahili kuwa katika
mpango huo.
Alisema wilaya za Kinondoni na
Temeke zimeshapokea malipo ya awamu saba ambayo ni Sh bilioni 6.7. Alisema hadi
sasa kuna kaya 32,456 zilizoondolewa kwenye mpango huo.
Kwa wastani kaya moja hulipwa kati
ya Sh 20,000 hadi 60,000 kwa kutegemea idadi ya watu katika kaya.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa alisema
mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, lakini kuna watu wanaoharibu
taswira ya Tasaf.
Alisema kuna fedha nyingi ambazo
zinaishia kwenye mikono ya wajanja na haziwafikii walengwa wa mpango huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema mpango huo umeandaliwa kitaalamu
na utaendelea kuwa endelevu na kwamba mradi huo unategemea zaidi serikali na
wafadhili, lakini hadi sasa kiasi kikubwa kimekuwa kikitoka kwa wafadhili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na
Utawala bora Mh. Angela Kairukia akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni,akiendelea na ziara katika Mkoa wa Dar es salaam kukagua maendeleo ya
mradi wa kusaidia kaya masikini TASAF
No comments:
Post a Comment