Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kuwa
Rais Dkt John Pombe Magufuli amempigia simu na kumwambia kuwa ana imani
naye na kuwa hajafikiria kutengua uteuzi wake labda kumpandisha cheo.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa
wa Arusha, Mrisho Gambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
baada ya taarifa kuhusu Rais kutengua uteuzi wake kusambaa kwenye mitandao ya
kijamii.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa alipigiwa
simu nyingi na watu wengi lakini kabla hajawajibu Rais Magufuli akampigia simu
na kumueleza kuwa ana imani naye na kuwa ahakikishe anawatumikia wananchi wa
Arusha kwani yeye sio bosi wao bali ni mtumishi wao.
Pia mkuu wa mkoa alieleza kuwa Rais
amempa maagizo ya kuhakikisha anasimamia wananchi wa mkoa wa Arusha walipe kodi
kwa ajili ya maendeleo ya mkoa huo na nchi kwa ujumla.
Aidha, ili kuthibitisha kuwa ni
Rais Magufuli ndiye aliyempigia simu, Rais aliomba kuongea na yeyote aliyekuwa
karibu ndipo mkuu wa mkoa akampa mmoja wa waliokuwa katika mkutano huo
kuthibitisha kuwa ni Rais Magufuli.
Habari ya kutenguliwa kwa mkuu wa
mkoa wa Arusha imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kuibuka mvutano mkali
kati ya mkuu huyo wa mkoa na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuhusu mradi
wa ujenzi wa hospitali itakayotoa huduma kwa mama na mtoto mkoani humo.
No comments:
Post a Comment