Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema hati ya shamba lililopo maeneo ya
Bunju la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick
Sumaye liko katika hatua ya kufutwa na kwamba Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya
Kinondoni Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi ya siku 90.
Lukuvi ameyasema hayo jana jijini
Dar es Salaam wakati akizungumza na wandishi wa habari.
“Shamba la Sumaye hati yake iko
katika hatua za kufutiwa,
Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ambaye
anajukumu la kutoa notisi, ameshatoa notisi kwamba hajaendeleza eneo hilo kwa
muda mrefu hivyo kwa mujibu wa sheria hati yake inatakiwa kufutwa,” alisema.
Alisema serikali haitofumbia macho
wamiliki wa ardhi na mashamba ambao hawajayaendeleza kwa muda mrefu.
Pia, kufuatia ongezeko la matapeli
wanaotumia nyaraka za kughushi za barua za toleo (ofa) zinazodaiwa kutolewa na
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Lukuvi alitoa agizo hususani kwa wakazi
wa jiji hilo wanaomiliki ardhi pasipo kuwa na hati miliki, kujisalimisha kwa
kupeleka barua zao za ofa kwa Kamishna wa Ardhi ili wapatiwe hati halali.
“Wamiliki wote wanaomiliki ardhi
kwa karatasi za ofa halali wazibadilishie ili wapewe hati halali, na
atakaegundulika kumiliki ofa feki polisi watawakamata na kupelekwa mahakamani,” alisema.
Alisema asilimia 60 ya watu
wanaopeleka kesi za migogoro ya ardhi wizarani, chanzo cha migogoro hiyo ni
karatasi za ofa zinazotoka katika halamshauri za jiji na manispaa.
“Natoa miezi mitatu ili karatasi
hizi zisitokee tena kila mtu alete barua ya ofa watapewa hati zao ndani ya
mwezi mmoja ,wazilete kwa kamishna wa ardhi wa mkoa, baada ya hapo sitasikiliza
malalamiko ya watu walioibiwa ardhi wakiwa na ofa ya namna hii.
“Tumieni miezi mitatu vizuri
kubadilisha ofa,” amesema.
Hali kadhalika, Lukuvi alipiga
marufuku vitendo vya uvamizi wa ardhi na mashamba vinavyofanywa na baadhi ya
wananchi, na kuwataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna
shamba au ardhi isiyoendelezwa.
“Serikali ina laani uvamizi wa
ardhi na mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi sababu baadhi yao
yanamilikiwa kihalali na yana hati, serikali ipo na sheria zipo zitafanya kazi
yake,” alisema.
No comments:
Post a Comment