Viongozi wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) wamekimbilia mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa
umeya na naibu meya wa Manispaa ya Kinondoni katika Jiji la Dar es Salaam
uliompa ushindi Diwani wa Msasani, Benjamin Sitta wa CCM kuwa Meya.
Ukawa kupitia kwa Wakili wao, John
Mallya wamewasilisha kesi hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 23 mwaka huu, kwa kuwa
ulikuwa batili na ulikiuka taratibu za kisheria.
Mallya alisema kesi hiyo ambayo
walalamikaji ni aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Jumanne Mbunju na
aliyekuwa mgombea wa umeya, Diwani wa Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro,
imepokelewa lakini haijafunguliwa.
Mbali na Sitta, walalamikiwa
wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya, Manyama Mangaru, Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa
Halmashauri hiyo.
Akizungumza baada ya kesi hiyo
kupokelewa, Wakili Mallya alisema wamefungua kesi hiyo kupinga kile wanachoita
uchaguzi ambao CCM walikaa wenyewe na kupigiana kura.
Alisema: “Katika kesi hiyo
tunaiomba Mahakama itengue uamuzi uliomchagua meya huyo, iamuru manispaa
iitishe uchaguzi wa umeya mara moja pia imuamuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa na wasimamizi wa uchaguzi wafuate taratibu za kisheria.”
Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es
Salaam, Henry Kileo alisema wamefika mahakamani kutafuta haki kwa sababu
wanaamini wamenyang’anywa haki yao.
Alisema kilichosababisha uchaguzi
wa Ubungo kuahirishwa ni kukiukwa kwa taratibu hivyo Mkurugenzi na Ofisa Tawala
wa Ubungo walipoona taratibu zimekiukwa Kinondoni, waliamua kuahirisha
uchaguzi.
“Kilichofanyika siku ile ilikuwa ni
kuchagua Mwenyekiti wa CCM, lakini siyo uchaguzi wa kumchagua meya wa Kinondoni
kwa sababu hata kisheria, uchaguzi unatakiwa kuwa robo tatu ya wajumbe ambao
walitakiwa kuwa 23, lakini walikuwa 18, ndiyo maana hata matokeo yalikuwa kura
18,” alisema.
Alidai madiwani wao walinyimwa
fursa ya kuingia manispaa na kuwasilisha malalamiko yao hivyo hawamtambui Meya
wa Kinondoni na kwa sasa hakuna Meya wa Manispaa hiyo.
No comments:
Post a Comment