Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia raia wawili wa
China kwa tuhuma za kumteka nyara Mchina mwenzao, Liu Hong (48) ambaye ni
mfanyakazi wa Le Grande Cassino, wakidai kulipwa dola za Marekani 19,000 (zaidi
ya shilingi milioni 38).
Akizungumza
na waandishi wa habari Jumatano hii,jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi
kanda maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro, alisema walipokea taarifa kwamba
raia huyo wa China alitekwa nyara na watu wasiofahamika.
“Oktoba 24, mwaka huu saa 11 jioni
kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha polisi kanda maalumu walibaini
kuwa wateka nyara hao wapo katika hoteli ya Palm Beach Upanga na walipofika
hapo wakaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine,” alisema Kamanda Sirro.
Aidha kamanda Sirro alisema,
“Polisi walipofika chumba namba tisa na kugonga wahusika waligoma kufungua
mlango ndipo polisi waligundua wateka nyara hao kuwepo katika chumba hicho.
Wakiwa wanajiandaa kuvunja mlango, mara mtuhumiwa mmoja Wang Young Jing (37)
raia wa China aliamua kufungua mlango na kumkamata akiwa na Liu ambaye ni
mtekwa nyara.”
“Askari walipoingia ndani walimkuta
aliyetekwa nyara akiwa hajitambui akiwa na majeraha usoni. Pia katika tukio
hili, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine aitwaye Chen Chung Bao
(35) raia wa China ambaye ndiye aliyekodi chumba hicho,” alieleza kamanda.
“Ndani ya chumba hicho kulikutwa
vipande viwili vya taulo walivyotumia kumfunga mikono, kamba za plastiki na
bomba la sindano. Alisema majeruhi alipelekwa katika hospitali ya taifa
Muhimbili kwa matibabu na watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa. Upelelezi
utakapokamilika watafikishwa mahakamani,”aliongeza.
Alisema taarifa hizo zilieleza
kwamba Liu alitekwa nyara Oktoba 23, mwaka huu saa moja asubuhi na ndipo polisi
wakaunda kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini
watekaji walikuwa wakidai Yen 100,000 (fedha za China) ambazo ni sawa na dola
za Marekani 19,000.
BY: EMMY MWAIPOPO
No comments:
Post a Comment