Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
umeingia kwenye jaribio jingine, baada ya Wazanzibari 40,000 kufungua kesi
mahakamani kupinga uhalali wake.
Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) na Rashid Salum Adiy kwa niaba ya
wenzake 39,999, katika Masijala ndogo ya mahakama hiyo iliyoko jijini Dar es
Salaam.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Adiy anasema kuwa msingi wa
kesi hiyo ni kwamba Muungano huo haukuanzishwa kisheria.
“Sisi tunadai Muungano huu hauko
kwa misingi ya kisheria na kutokana na ushahidi tulionao, uko kisiasa tu na
jambo hili linahitaji mfumo na mwenendo wa kisheria kwa kuwa wenye mamlaka ya
nchi ni wananchi,”alisema Adiy.
Alisema kutokana na nyaraka walizonazo
wanapinga hati ya Muungano inayodaiwa ilisainiwa Aprili 22, 1964 na wanapinga
uamuzi wa Baraza la Mapinduzi kuridhia Muungano huo.
Wanapinga barua ya Mei 6, 1964,
iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kuelezea kutambuliwa kwa
Muungano huo.
Pia, wanapinga uhalali wa barua ya
Novemba 2, 1964 iliyopelekwa UN ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Sheria iliyopitishwa na Bunge Desemba 10, 1964
ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Adiy na wenzake wanadai kwa kuwa
Muungano ni wa kisiasa, ndiyo maana hauwezi kuleta manufaa kwa pande zote mbili
hususani uwiano wa kiuchumi na kielimu.
Baada ya kuwasilisha nyaraka zao
wanasubiri kesi hiyo isajiliwe kwa kupewa namba katika Mahakama hiyo na
kupangiwa taratibu za usikilizwaji wake.
Mbali na Wazanzibari 40,000, pia
alisema wanayo majina mengine ambayo watayawasilisha mahakamani baadaye, kesi
itakapokuwa imeanza
No comments:
Post a Comment