Watanzania wanakumbuka kuwa mnamo
tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la ardhi katika eneo la Kanda ya
Ziwa na hususan Mkoa wa Kagera.
Tetemeko hilo lilisababisha athari
mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma
na watu binafsi. Jumla ya Watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao,
mali na athari za kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba,
Karagwe na Kyerwa.
Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza
maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile, nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa
na nyumba 14,595 za makazi zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa
na hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya
yalisababisha uharibifu mbalimbali wa miundombinu ya barabara na majengo ya
watu na taasisi mbalimbali, ikiwemo shule na Hospitali.
Kufuatia maafa hayo, wananchi na
taasisi mbalimbali, pamoja na nchi marafiki, waliitikia wito wa kuwasaidia
wahanga wa maafa na kukarabati miundo mbinu iliyoharibika. Hadi kufikia mwezi
Oktoba, Fedha, Vyakula na Vifaa mbalimbali vya Ujenzi vilikuwa vimepatikana kwa
njia ya michango mbalimbali.
Chama chetu kimeshtushwa na kauli
ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwamba Wananchi walioathirika wajitegemee wenyewe na
kwamba misaada yote iliyotolewa Ni ya Serikali na Taasisi zake tu. Kauli hii ya
Mkuu wa Mkoa haikubaliki kwani inadhalilisha waathirika na watu wote waliojitoa
kuwasaidia waathirika hao.
Tunachukulia kauli hii kama tangazo
la wizi wa uaminifu wa wananchi waliochanga. Ni busara ya kawaida kuwa hatua ya
kwanza katika kushughulikia maafa ni kurudisha hali ya maisha ya watu katika
hali ya kawaida sambamba na ukarabati wa miundombinu. Aidha, suala la ujenzi wa
miundo mbinu ya taasisi za umma ni jukumu la msingi la serikali. Kwa sababu
hii:
• ACT Wazalendo tunaitaka serikali
kuu kujitenga na kufuta kauli ya mkuu wa mkoa wa Kagera kwa sababu
inaigombanisha serikali na wananchi inaowaongoza.
• ACT Wazalendo tunaitaka serikali
kuelekeza ni misaada iliyopatikana kwa michango ya wananchi, taasisi na nchi
rafiki katika kusaidia wananchi walioathirika kurudi katika maisha ya kawaida,
ikiwemo ukarabati na ujenzi wa nyumba za kuishi.
• ACT Wazalendo tunatoa wito kwa
taasisi za kiraia nchini kuchukua nafasi yake katika kuendelea kuikumbusha
serikali wajibu wake wa msingi wa kuboresha maisha ya watu.
Janeth Rithe
Katibu wa Taifa ACT Wazalendo,
Kamati ya Maendeleo ya Jamii
13/11/2016, Dar Es salaam.
No comments:
Post a Comment