Wakati Mbunge wa Arusha Mjini
(Chadema), Godbless Lema (40) akitarajia kujua hatima ya dhamana yake katika
Mahakama Kuu leo, kesho yeye na mkewe Neema Lema (33) watapanda kizimbani kwa
kesi ya uchochezi dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Ijumaa iliyopita Lema alipelekwa
Gereza la Kisongo, Arusha baada ya kunyimwa dhamana katika kesi nyingine ya
kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, hatua ambayo imepingwa na
chama chake na mawakili wake.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha,
Calist Lazaro alisema hawakuridhishwa na pingamizi la dhamana lililowekwa na
mawakili wa Serikali kwani tayari Lema alikuwa amepewa dhamana na Mahakama ya
Hakimu Mkazi.
“Tayari tumefanya mazungumzo
kuongeza nguvu za mawakili wa chama ambao wataungana na mawakili wa Arusha
kudai dhamana leo,”alisema.
Mmoja wa mawakili hao, Shaki
Mfinanga alisema leo wanatarajia kuwasilisha maombi ya dhamana ya Lema wakiwa
na mawakili wa Chadema.
Kesi ya mkewe
Wakati hayo yakiendelea, kesho Lema
na mkewe watakuwa mahakamani mbele ya kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa
Arusha, Desdery Kamugisha.
Katika kesi hiyo, Hakimu Kamugisha
amewapa dhamana washtakiwa hao katika kesi ya kusambaza ujumbe kumkashifu mkuu
wa Mkoa Arusha.
Lema anadaiwa kuwa Agosti 20, 2016
akitumia simu namba 076415**47 ambayo imesajiliwa kwa jina la mkewe, alituma
ujumbe kwenye namba ya Gambo 0766 75**75 wenye maneno ya uchochezi.
Maneno hayo; “Karibu
Tutakudhibiti kama Uarabuni walivyodhibiti Mashoga” yanadaiwa ya
uchochezi kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Kifungu cha 118 (a) na
Kifungu cha tatu katika sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Katika shtaka jingine, Lema
anashtakiwa peke yake, akituhumiwa kivunja Sheria ya Makosa ya Jinai namba 390
kifungu cha 35 kwa kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria wakati wa mkakati
ulioitwa Ukuta na chama hicho.
Lema alidaiwa kutenda kosa hilo
kati ya Agosti Mosi hadi 26 kwa kusambaza ujumbe kupitia mtandao wa WhatsApp
wakati akijua kufanya ni kosa kisheria. Katika kesi hiyo, Lema na mkewe
wanatetewa mawakili wanne, John Mallya, James Lyatuu, Reygod Nkya na Mfinanga.
No comments:
Post a Comment