Mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Anne Makinda amezishauri hospitali, vituo vya afya
na zahanati za serikali kuboresha huduma za afya ili wananchi waliojiunga
katika mifuko ya afya ya jamii (CHF) na mfuko wa bima ya afya washawishike
kutumia huduma katika hospitali zao.
Makinda ametoa rai hiyo jana
alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kujionea huduma za Bima ya
afya zinavyotolewa na changamoto zilizopo ili kwa ushirikiano wa mfuko wa bima
ya afya na wadau wake waweze kuzitatua.
Alisema hospitali na vituo binafsi
au vya mashirika mbalimbali wamekuwa wanufaikaji wakubwa wa kupata wateja wengi
wa bima ya afya na mifuko ya afya ya jamii kutokana na kusifiwa kuwa wanatoa
huduma bora tofauti na hospitali za serikali ambazo hupata wateja wachache na
hivyo kupata faida kidogo.
Makinda alisema hamasa anayoitoa ya
kuboresha huduma kwa vituo vya serikali haimaanishi mfuko wa taifa wa bima ya
afya hauthamini vituo na hospitali binafsi bali inataka hospitali za serikali
kuboresha huduma na kuingia katika ushindani.
Aliongeza kuwa changamoto ya
ukosefu wa dawa na vifaa tiba inawakatisha tamaa watumiaji wa bima ya afya
pamoja na watu wengine kujiunga hata hivyo mfuko wa bima ya afya na hospitali
za serikali zimejipanga kuziondoa changamoto hizo.
Aidha Makinda aliupongeza Mkoa wa
Singida kwa kufanya vizuri katika mfuko wa afya jamii na bima ya afya huku
akisisitiza kuendelea kuboresha ili Mkoa wa Singida uwe mfano kwa mikoa mingine
ya Tanzania.
Akitembelea majengo mapya ya hospitali
rufaa iliyopo eneo la Mandewa Makinda alivutiwa sana na majengo hayo huku
akiutaka uongozi wa Mkoa kwa kushirikia na wadau wengine hasa mfuko wa bima ya
afya kutafuta pesa za ukamilishaji wa majengo muhimu ili huduma zianze kutolewa
katika hospitali hiyo kwakuwa itakuwa msaada hata kwa kanda nzima ya kati.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida
Mheshimiwa Mhandisi Mathew J Mtigumwe alimshukuru Anne Makinda kwa kuutembelea
mkoa wa Singida ili kujionea huduma za Bima ya afya zinavyotolewa.
Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe
alimuahidi Makinda kuwa Mkoa utaendeleza ushirikiano mzuri na Mfuko huo na
kuomba waendelee kutoa ushirikiano wa vifaa tiba na ukarabati wa miundombinu ya
hospitali na vituo vya afya vya serikali ili kuboresha huduma za afya Mkoani
Singida.
Aliongeza kuwa Mkoa utaendelea
kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na bima ya afya ili
wapate huduma bora hata wakati wakiwa na upungufu wa fedha kwani bima huokoa
maisha
No comments:
Post a Comment