Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika mradi
mkubwa wa maji kwenye mji Nansio katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza mradi
ambao utahudumia wananchi elfu 61.
Makamu wa Rais ambaye jana
alisafiri kwa takribani masaa Matatu na meli ya MV Nyehunge II katika Ziwa
Victoria kwenda kisiwa hicho kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa
huo,aliwahimiza wananchi hao wautunze mradi huo ambao utasaidia kwa kiasi
kikubwa kuondoa tatizo na uhaba wa maji safi na salama katika kisiwa hicho.
Mradi huo ambao unaojumuisha kazi
za uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira unatekelezwa chini ya
umefadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na serikali ya Tanzania
katika miji ya Sengerema,Geita na Nansio – Ukerewe kwa gharama ya Dola za
Kimarekani milioni 30.4 ambapo serikali ya Tanzania imechangia mradi huo Dola
za Kimarekani milioni nne.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
aliwaahidi wananchi kuwa serikali ya awamu ya Tano inamikakati mizuri
inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao
hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta
maji.
Akihutubia mamia ya wananchi
wa kisiwa cha ukerewe kwenye kijiji cha Kagunguli mkoani Mwanza mara baada ya
kuweka mawe ya msingi katika miradi miwili ukiwemo mradi wa maji na
ujenzi wa chumba cha upasuaji katika kituo cha afya cha Kagunguli, Makamu wa Rais
aliwapa pole wananchi wa kisiwa hicho baada ya kukumbwa na tufani ya kimbunga
cha upepo iliyotokea tarehe 04 Novemba 2016 na kusababisha uharibifu mkubwa
ikiwemo nyumba za watu kubomoka.
No comments:
Post a Comment