Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB), imetangaza siku 90
kuanzia Oktoba 31 mwaka huu kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo
2016/2017 kukata rufaa kwa njia ya mtandao ikiwa hawajaridhishwa na matokeo ya
upangaji uliotangazwa hivi karibuni.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu hii na mkurugenzi mtendaji wa HESLB
Abdul-Razaq Badru, Bodi imeanza kupokea rufaa hizo kwa njia ya mtandao (Online
Loan Application and Management System) kuanzia Oktoba 31 hadi Januari 31,
2017.
“Wanachotakiwa kufanya wanafunzi ni
kuingia katika mtandao wetu wa http://olas.heslb.go.tz na kujazafomu, kuichapa
na kuiwasilisha kwa afisa mikopo wa chuo chake ambaye atawasilisha kwetu fomu
zote za chuo chake kwa barua kwa ajili ya sisi kuzifanyia kazi,” amesema Badru.
Katika taarifa yake ya mkurugenzi
mtendaji huyo inayopatikana pia katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz)
ameongeza kuwa Bodi haitapokea wala kuzifanyia kazi fomu za rufaa ambazo
zitawasilishwa Bodi na wanafunzi bila kupitia kwa maafisa mikopo wa vyuo vyao.
Serikali imetenga shilingi bilioni
483 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi 119,012 kati yao wanafunzi
93,295 wanaondelea na masomo na wanafunzi 25,717 ni wa mwaka wa kwanza. Hadi
sasa, jumla ya wanafunzi 20,183 wa mwaka wa kwanza wameshapata mkopo.
BY: EMMY MWAIPOPO
No comments:
Post a Comment