Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
imesitisha kuweka dhahabu kama hazina ya rasilimali za kigeni kwa sababu ya
kuyumba kwa bei ya madini hayo katika soko la dunia na kusababisha uwezekano wa
kupunguza thamani ya hazina ya rasilimali ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Ashatu Kijaji alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Igunga Mhe. Dalaly Kafumu aliyehitaji kufahamu
sababu za Serikali kukataa kutunza dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania
ni nchi mojawapo inayozalisha dhahabu safi.
Mhe. Kijaji alisema kuwa jukumu la
msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kuwa na
utulivu wa bei kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa hivyo ili
kufanikisha azma hiyo Benki Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa
kutumia nyenzo mbalimbali zikiwemo za kuuza dhamana na hati fungani za Serikali
pamoja na kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki.
“Katika kutekeleza jukumu lake la
msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza
bidhaa nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne lakini kwa muda mrefu sasa
Benki Kuu ya Tanzania haiweki dhahabu kama sehemu ya rasilimali hizo kutokana
na kuyumba kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia”, alisema Mhe.
Kijaji.
Naibu Waziri huyo alitoa mfano wa
kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la Dunia ambapo dhahabu ilishuka kutoka
dola 1,745 za kimarekani katika mwezi Septemba 2012 hadi dola za kimarekani
1,068 kufikia mwezi Desemba 2015.
Mhe. Kijaji alifafanua kuwa hazina
ya rasilimali za kigeni zinaweza kuwa dhahabu – fedha (monetary gold) au fedha
za kigeni ambapo uamuzi kuhusu hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo
mbalimbali vikiwemo vile vya kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha pamoja na
faida inayopatikana kwa kuwekeza hazina hiyo.
Aidha, Mhe. Kijazi alisema kuwa
ununuzi na uuzaji wa madini ya dhahabu unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa
kuzingatia jukumu la msingi la Benki Kuu inaonyesha dhahiri kuwa Benki hiyo
haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya madini hayo.
No comments:
Post a Comment