Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ameibuka na
kutaja utatu unaojumuisha mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba,
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Jeshi la Polisi akieleza
ndio unaoshirikiana kukihujumu chama hicho, huku akibainisha mambo tisa
anayoeleza kuwa ‘ushahidi wa ushirikiano’ na hujuma hizo.
Akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuibuka kwa
mgogoro ndani ya chama hicho baada ya Jaji Mutungi kumtambua profesa Lipumba
kuwa mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif alitumia dakika 95 kueleza hujuma
hizo na kudai zinalenga kukifanya chama hicho kutodai haki ya kunyang’anywa
ushindi wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.
Akiwa sambamba na viongozi mbalimbali wa chama hicho, alisema
hana ugomvi na Profesa Lipumba na yupo tayari kukaa naye meza moja kueleza
uongo wa mtaalamu huyo wa uchumi, ikiwa ni pamoja na ukweli anaouficha kuhusu
kujiuzulu kwake uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana na uamuzi wake wa kutaka
kurejea katika chama hicho.
Mbali na kukiri CUF kupitia katika wakati mgumu kwa sasa, Maalim
Seif alisema hujuma hizo zilizotokana na ‘wakubwa’ kuchukizwa na kitendo cha
chama hicho kuwasilisha vielelezo Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC)
vinavyowatuhumu viongozi wa Serikali kutumia mamlaka yao vibaya katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka
jana, zimesababisha chama
hicho kutopata ruzuku ya Sh milioni 117 kila mwezi, tangu Agosti mwaka huu.
“Mtiririko wa matukio haya (tisa)
yanaonesha wazi hujuma hizi…, ni mambo yanayoratibiwa kwa
suhirikiano wa makusudi kati ya msajili, polisi na Lipumba, “ alisema
Maalim Seif.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni
kuvamiwa kwa Mkutano Mkuu wa CUF iliofanyika Agosti 21, utekaji wa wanachama na
viongozi wa chama hicho, kuvamiwa kwa ofisi kuu iliyopo Buguruni, kuvunjwa kwa
ofisi za wilaya ya Bagamoyo na Mkuranga, wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la chama hicho kuzuiwa kufanya kikao cha ndani.
Mengine ni kuzuiwa kufanyika kwa
mkutano mkuu maalumu wilaya ya Tanga, utekaji wa mlinzi wa chama hicho
uliofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuzuiwa kwa kikao cha ndani
mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa Profesa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa
CUF kuingia chumba cha mahakama kuu hiyo.
Agosti 8 mwaka jana Profesa Lipumba
alitangaza kuachana na uongozi wa chama hicho, baada ya CUF kukubaliana na
Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa kuwania urais.
Hata hivyo, Juni mwaka huu Profesa
huyo aliomba kwa barua kurejea kwenye wadhifa wake, ambao kwa sasa unashikiliwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro aliyechaguliwa katika
mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.
Uamuzi wake huo ulizua
sintofahamu ndani ya CUF huku mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho
uliofanyika Agosti 21 mwaka huu kumchagua mwenyekiti mpya ukivunjika baada ya
kundi la wafuasi wa chama hicho kuvamia na kufanikiwa kuzima mchakato wa kupiga
kura kumchagua mwenyekiti mpya, wakishinikiza Profesa Lipumba aruhusiwe kurejea
katika wadhifa huo.
Baada ya sakata hilo Baraza Kuu la
Uongozi la chama hicho lilimvua uanachama Profesa Lipumba na kuwasimamisha
uanachama makada kadhaa wa CUF, jambo ambalo liliingiliwa kati na Msajili wa
Vyama vya Siasa aliyetoa waraka wa kumtambua Lipumba kuwa mwenyekiti.
Kitendo cha Lipumba kutambuliwa na
kurejea katika chama hicho kilisababisha Baraza la Wadhamini la CUF kufungua
kesi Mahakama Kuu na kumshtaki profesa huyo Jaji Mutungi na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.
Katika ufafanuzi wake, Maalim Seif
alisema Lipumba alivamia Mkutano Mkuu wa chama hicho akiongozwa na polisi na
kusababisha vurugu kubwa sambamba na uharibifu wa mali lakini polisi
haikuchukua hatua yoyote.
“Kumekuwa na matukio kadha aya
utekaji wa viongozi na wanachama wa CUF…, mkurugenzi wetu wa fedha Joram
Bashange alitekwa akiwa anatoka nyumbani kwake na walinzi wa Lipumba, licha ya
kukamatwa na kufikishwa polisi waliachiwa na gari walilotumia nalo halipo kituo
cha polisi buguruni,” alisema.
Alisema Septemba 24 mwaka huu,
Lipumba na wafuasi wake walivamia ofisi kuu ya CUF iliyopo Buguruni na kufanya
uharibifu huku akipewa ulinzi mkali wa polisi.
“Polisi kazi yao ni ulinzi wa raia
na mali zao pamoja na kupambana na wahalifu lakini hivi sasa wao ndio wanatetea
wahalifu. Tunamuomba Mwigulu (Nchemba-Waziri wa Mambo ya Ndani) kuingilia kati
na kutizama watendaji walio chini ya wizara yake,” alisema
Maalim Seif.
Alisema tukio la nne ambalo polisi
imeshindwa kukamata wahusika licha ya kuwajua ni uvamizi uliofanywa na wafuasi
wa Lipumba wa kuvunja ofisi za chama hicho wilayani Bagamoyo na Mkuranga.
“Wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu
la uongozi la chama walizuiwa kufanya kikao cha ndani Newala na kukamatwa
walipokuwa Nachingwea,” alisema na kubainisha kuwa wakati viongozi hao
wakikamatwa, Lipumba anafanya vikao kama hivyo bila kukamatwa.
“Polisi walizuia kufanyika kwa
mkutano mkuu maalum wa wilaya ya Tanga kwa madai kuna pande mbili zinavutana.
Pia Novemba 10 mwaka huu mlinzi wa chama, Mohamed Said alitekwa akiwa mahakama
kuu na kupigwa sana na kunyang’anywa fedha na kupelekwa kuhojiwa na Lipumba.
Tukio hilo lilitokea mbele ya polisi,” alisema.
Alisema jeshi hilo pia lilizuia
kufanyika kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa Lipumba kutaka
kuzuia viongozi wa CUF kuingia ndani ya chumba cha mahakama kufuatilia shauri
lao, huku akimtaja mmoja wa walinzi hao kuwa ni Hassan Kingwele.
Akijibu hoja mbalimbali
zilizoibuliwa na Lipumba, Maalim alisema msomi huyo anatumiwa na dola na
kubainisha kuwa anaficha ukweli juu ya uamuzi wake wa kujiondoa CUF.
“Lipumba bado hajasema sababu za
kweli juu ya kujiuzulu kwake, yeye ndio alikuwa mwanzilishi wa Ukawa katika
Bunge Maalum la Katiba na ndio aliyemtafuta Lowassa na kumshawishi awanie urais
kupitia Ukawa,” alisema.
“Lowassa ilikuwa ajiunge na NCCR
kwa sababu ni chama kidogo ili CUF na Chadema tumuunge mkono kwa mantiki hiyo
iweje Lipumba aseme mimi sikumshirikisha ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa?”
Alisema yeye hana ugomvi na Lipumba
bali mtaalam huyo wa uchumi ana ugomvi na CUF, huku akidai kuwa hivi sasa
anatumia udini, ukabila na uzanzibari kukigawa chama hicho.
“Hizi ni jitihada za dola kunifanya
nisidai haki kwa yaliyotokea Zanzibar…, hilo halitawezekana nitaidai tu mpaka
mwisho,” alisema.
No comments:
Post a Comment